Huyu ni Mchungaji Msigwa `orijino’ wa CHADEMA au…

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:09 AM Jun 05 2024
Mchungaji Peter Msigwa

MEI 29 mwaka huu, CHADEMA, Kanda ya Nyasa, ilifanya uchaguzi wa mwenyekiti wake wagombea wakiwa ni Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Mchungaji Peter Msigwa ambaye alikuwa anatetea nafasi hiyo.

Baada ya kupiga kura kulichofanyika Makambako mkoani Njombe, Sugu aliibuka kidedea kwa kupata kura 54 ambazo ni sawa na asilimia 51, huku Mchungaji Msigwa akipata kura 52 sawa na asilimia 49.
 
 Baada ya matokeo kutangazwa, Mchungaji Msigwa anakaririwa na vyombo vya habari akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wagombea wote ambao kura hazikutosha, akimpongeza Sugu kwa ushindi huo.
 
 Alikaririwa akisema hiyo ndiyo demokrasia na nafasi hizo ni za kubadilishana. "Nawashukuru sana viongozi wote wa mkutano huu, kura ndizo zimeamua hivyo mmepata mlichokitaka na nikupongeze Sugu kwa kupata nafasi hiyo, mimi sikuja kwenye chama hiki ili kutaka cheo."
 
 Pia, anaongeza hapo  akiahidi kwamba ataendelea kuwa mwanachama na kwamba yeyote anayehitaji ushauri kwa chochote yuko tayari na kwamba wazidi kushirikiana na kuongeza kuwa hahitaji cheo ili kuwa bora.
 
 Hata hivyo, siku chache baada ya kutoa maneno hayo, Mchungaji Msigwa ameibuka upya akipinga matokeo akirusha tuhuma ambazo anadai zilisababisha ashindwe katika uchaguzi huo.
 
 Lakini, kabla ya kuendelea, ninaomba ieleweke kuwa hapa siyo kupinga tuhuma anazotoa Msigwa, kwa sababu yeye alikuwa kwenye eneo la tukio, bali ninachokieleza ni kwa nini anatoa kauli zinazopingana kwa suala moja?
 
 Ina maana Mchungaji Msigwa aliyekaririwa akipongeza na kuahidi kutoa ushirikiano baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa ni mwingine na huyu ambaye sasa anapinga uchaguzi huo ni mtu mwingine?
 
 Hivi baada ya matokeo alishinikizwa kupongeza au kushukuru? Kwa nini sasa abadilike aje na kauli nyingine tofauti na ile ya awali?  Au ndiyo kauli ambazo zimekuwa zikisemwa kuwa 'usimwamini mwanasiasa'? 
 
 Kwa sasa amekata rufani kupinga matokeo ya uchaguzi uliompa ushindi Sugu, anadai kuwa katika uchaguzi huo kulikuwa na ukiukwaji wa kanuni za katiba katika upigaji kura pamoja na kufanyika kwa fujo ambazo zilichangia kuharibu uchaguzi huo.
 
 Mbali na kukata rufani anasema, kama chama kitashindwa kufanyia kazi barua yake ya kukata rufani, kitashindwa kujitofautisha na CCM katika kuminya demokrasia na haki.
 
 Vilevile, anakishauri chama chake kijitafakari upya na kurudi katika misingi yake ya haki na demokrasia kwa kuheshimu mawazo ya watu wote wakiwamo wanachama, bila kuwapinga na kuwapuuza kwa kuwa kupishana kwa hoja ndio ukomavu wa kisiasa.
 
 Kimsingi ushauri wake ni wa muhimu, lakini swali langu ni kwamba kwa nini alipongeza uchaguzi huo na sasa anageuka na kupinga matokeo? Kwa nini hakupinga wakati matokeo yanatangazwa?
 
 Huyu ni Mchungaji Msigwa mwingine wa CHADEMA au yule yule aliyekubali matokeo na kuahidi kutoa ushirikiano kwa mpinzani wake? Kwa nini abadilike ghafla na kuja kivingine?
 
 Ninadhani ipo haja kwa wanasiasa kujenga mazingira ya kuaminika, kwani utata wa kauli zao umekuwa ukisababisha baadhi ya watu waseme kuwa wanasiasa si wa kuaminika wanabadilika wakati wowote.
 
 Kwa tuhuma anazotoa kwa sasa, maana yake ni kwamba kauli yake ya kwanza ilikuwa si ya kweli na sasa ndio anasema ukweli wa kile kilichotokea katika uchaguzi huo? Binafsi na hata wana CHADEMA wengine ametuacha njia panda. 
 
 Ninaamini kwamba wale wote walisikia kauli ya kwanza, watakuwa wameshindwa kuelewa ni kwa nini sasa ameibuka na tuhuma ambazo angezitoa tangu mwanzo badala ya kutoa neno la shukrani. 

Kwa hali hiyo nina neno kwa CHADEMA ushauri wangu kumbuke hayo si mazuri kwenye kusherehekea uhuru wa kutoka kifungoni baada ya miaka saba ya vitisho kwa vyama vya upinzani na kuzuiliwa kufanya kazi zenu na serikali ya awamu ya tano.