HESLB itimize ushauri huu

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:33 AM May 29 2024
HESLB.
Picha: Mtandaoni
HESLB.

HIVI karibuni iliibuliwa hoja bungeni, kuhusu utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kwamba serikali iwafuatilie mitaani kubaini idadi ya vijana walioacha kuendelea na masomo ya vyuo vikuu na kurudi nyumbani kutokana na wazazi au walezi kushindwa kuwagharamia.

Mbunge wa Ngara, mkoani Kagera, Ndaisaba Ruhoro andiye mwenye hoja hiyo ambaye anaongeza kuwa serikali ikishawapata iwapeleke Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu  (HESLB) ili wapatiwe mikopo na kuendelea na masomo  ili kutimiza ndoto zao za kujiendeleza kielimu.
 
 Anasema, hali imekuwa mbaya zaidi kama ilivyo katika ngazi za chini, kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi kuacha masomo, na sasa  kibao kimegeukia upande wa vyuo vikuu, kwa wanachuo  kuacha masomo.
 
 Kwa hoja hiyo, ninaungana na mbuge huyo, kwani pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali kuboresha elimu, bado kumekuwapo na malalamiko kwenye suala la mikopo ya elimu ya juu.
 
 Imekuwa ikielezwa kuwa pamoja na serikali kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, wapo baadhi ya wanafunzi ambao wamekuwa wanakosa licha ya kuwa na vigezo vya kupata ufadhili huo.
 
 Nadhani wakati sasa wa HESLB kuhakikisha wanafunzi wanapata mikopo hiyo bila usumbufu, kwani lengo la bodi hiyo ni kuwezesha  kusoma elimu ya vyuo vikuu na vyuo vya kati.
 
 Nipashe ilishawahi kuzungumza na wanafunzi waliolalamika kunyimwa au kupatiwa mkopo 'kiduchu', lakini Mkuu wa Mawasiliano wa HESLB, Omega Ngole, akabainisha kuwa mwaka huu wa masomo, hakuna mwanafunzi aliyepatiwa mkopo kwa asilimia 100 isipokuwa waombaji wenye ulemavu na wale waliopoteza wazazi wote wawili.
 
 Uamuzi wa bodi wa kutoa mkopo wa asilimia 100 kwa wanafunzi wenye ulemavu na waliofiwa wazazi wote ni sawa, lakini inawezekana pia wapo baadhi ya wanafuzni wakawa na wazazi wote lakini hawana uwezo.
 
 Vilevile inawezekana baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu, wanatoka katika familia zenye uwezo, hivyo, ni vyema kuendelea kufuatilia hilo kwa karibu ili kupunguza idadi ya wanafunzi wanaokatisha masomo.
 
 Hivyo, litakuwa jambo jema iwapo kutakuwa na ufuatiliaji wa karibu suala hilo la mikopo ya elimu ya juu ili kama itawezekana, basi wanafunzi wote wapewe  ili waweze kutimiza ndoto zao katika elimu.
 
 Lakini pia, kwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alishasema serikali inakaribisha taarifa za wananchi kwa ajili ya uchunguzi unaoendelea kuhusu mchakato wa kutoa mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu, basi wajitokeza kusaidia katika hilo.
 
 Ni wakati akielezea uamuzi wa serikali kuunda timu ya kuchunguza mchakato wa utoaji wa mikopo, kwa ajili ya wanafunzi hao ili kubaini changamoto na kutoa ushauri.
 
 Kimsingi, lengo ni kuondoa changamoto katika utoaji wa mikopo hiyo kama zipo, na inawezekana kukawa na mawazo mazuri zaidi yatakayosadia kuboresha mikopo hiyo.
 
 Lakini pia, hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema serikali imeongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu kutoka Sh. bilioni 654 kwa mwaka 2022/23 hadi Sh. bilioni 738.7 mwaka 2023/24.
 
 Katika hilo wakati wa hotuba yake bungeni jijini Dodoma, alisema wanufaika wa mikopo na ruzuku wameongezeka kutoka  177,615 mwaka 2022/23 hadi wanafunzi 220,278 mwaka 2023/24.
 
 Ninaamini hatua inaweza kuwa inalenga kuhakikisha wanafunzi wote wananufaika na mikopo hiyo bila kuwaacha wengine nyuma kwa vigezo ambavyo wakati mwingine vinaweza kuwaumiza.