Yanga, Mashujaa mechi ya kiufundi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:38 PM Dec 19 2024
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic

BAADA ya kutoka katika mashindano ya kimataifa, mabingwa watetezi, Yanga wanatarajia kuwakaribisha Mashujaa FC kutoka Kigoma katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam huku makocha wakitamba utakuwa mchezo wa ufundi zaidi.

Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema ameiangalia vizuri Mashujaa na kubaini ni timu nzuri, hivyo inakwenda kuwakabili kwa tahadhari na watatumia mifumo tofauti katika mechi hiyo.

Ramovic alisema anaweza kubadilisha mfumo kutokana na mchezo utakavyokuwa unaendelea kwa lengo la kuhakikisha wanapata matokeo chanya.

"Najua tunatakiwa tuonyeshe sisi ni nani, kila timu tunaiheshimu na kila mechi tunakwenda kucheza kwa plani tofauti, tunahitaji kushinda na kukaa sehemu salama, kwa sababu mechi zimekuwa nyingi sasa za ligi kuu na timu zilizo juu zimekuwa zikipata ushindi.

Kama hatuweka mkazo, kupambana kwenye mchezo huwezi kushinda, kama huwezi kukimbia uwanjani kama una mpira na kumkimbiza mpinzani wakati hauna mpira, basi huwezi kufanya kitu, tumemuangalia mpinzani wetu na tunajua jinsi gani tunakwenda kupamba naye kimbinu na kifundi," alisema Ramovic.

Kocha huyo pia amewaomba wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa wavumilivu kwa sababu bado ana muda mchache sana tangu alipojiunga na katika kikosi hicho.

"Kama nilivyosema nimekuja hapa nina wiki tatu tu, sina 'pre season',nimekuta timu imepoteza wachezaji muhimu wanne kwa majeraha, haiwezi kuwa rahisi, lakini hakuna hata mmoja anayetaka kujua kuhusu hilo,wanachohitaji ni matokeo moja kwa moja, ukweli ni presha kubwa lakini kwangu ndicho kitu ambacho nimezoea kuishi, tupo hapa kufanya kazi ili tushinde mechi za Ligi Kuu, kuhusu Ligi ya Mabingwa si muda wake hivi sasa," alisema kocha huyo.

Naye Kocha Mkuu wa Mashujaa, Abdallah Mohamed 'Bares', alisema timu yake inazihitaji zaidi pointi tatu kwa 'udi na uvumba'.

"Utakuwa ni mchezo mkubwa, kwetu sisi ni muhimu, tunajua tunacheza na timu kubwa, iliyosheheni wachezaji bora, lakini sisi upande wetu tumejiandaa vizuri zaidi ukilinganisha na michezo yote iliyopita, tunahitaji pointi tatu ili tufike kule tunakotarajia.

Sina shaka utakuwa ni mchezo wa kimbinu zaidi na kiufundi, tunajua Yanga ni timu inayochezea sana mpira ina viungo wazuri, ila sisi ni timu ambayo tunabadilika kutokana na timu tunayocheza nayo kwa hiyo tunatakikisha tunawadhibiti katika maeneo hayo, mbinu nyingine si vyema sana kuisema hapa,"alisema.