WAKATI imemtambulisha rasmi winga mpya, Jonathan Ikangalombo, Yanga imesema itaongeza umakini na haitarudia makosa ya kukubali kupoteza mechi kwenye uwanja wa nyumbani kama ilivyotokea walipokutana na USM Algers ya Algeria mwaka juzi, imeelezwa.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara waliruhusu kichapo cha mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na ushindi wa bao 1-0 ugenini haukuwasaidia kubeba taji la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka juzi.
Yanga inatarajia kuwakaribisha MC Alger ya Algeria katika mechi ya mwisho ya Kundi A ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Ushindi wa aina yoyote utaipeleka Yanga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo wakati MC Alger inahitaji sare ili kusonga mbele katika mashindano hayo.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema kwa sababu wanahitaji matokeo ya ushindi tu katika mchezo huo, viongozi na benchi la ufundi linaipa umuhimu wa kipekee mechi hiyo huku wakiongeza umakini tofauti na wanachama na mashabiki wanavyofahamu.
Kamwe alisema Yanga inawaonya wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuondoa dhana kuwa mechi hiyo itakuwa rahisi kwa sababu wanakwenda kucheza dhidi ya timu ngumu na iliyoshikiliwa hatima yao.
"Kuna tabia nimeiona kwa Wanayanga siku hizi. Yaani tunazungumza kama vile hii mechi ni rahisi sana, au MC Alger ni timu nyepesi na hii mechi imeisha, tunakosea sana, ni mechi kubwa na inahitaji maandalizi ya kutosha. Katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya 'ndugu' yake huyu USM Alger, tulikuwa na mategemeo kama haya, tulidhani tutamfunga hapa na kwenda kupata sare ugenini, kule kujiamini kupita kiasi kulituponza na Waarabu watakatuadhibu. Wao wana faida hata sare inawabeba, naomba tuungane na kupeana sapoti kwa ajili ya kushinda mechi hii," alisema Kamwe.
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, alisema maandalizi yanaendelea vyema huku akiwataka wachezaji wake waingie uwanjani kama hawajawahi kufanya kitu katika michezo yote iliyopita.
"Tuna mlima katika mchezo wa mwisho, kwetu ni kama fainali, najua utakuwa mgumu lakini nina imani kwa namna wachezaji wangu wanavyoonekana wana njaa ya kusaka ushindi.
Tunatakiwa kuingia uwanjani tukijiona kama vile hatujafanya kitu, tunatakiwa kuongeza umakini katika mchezo huu wa mwisho," alisema Ramovic.
Kocha huyo alitoa siri ya kuwakataza wachezaji wake kushangilia kupita kiasi katika ilivyokuwa katika mechi iliyopita waliyocheza dhidi ya Al Hilal Omdurman ambayo walipata ushindi wa bao 1-0.
"Niliwazuia wachezaji wangu kushangilia kupitiliza mara baada ya mchezo dhidi ya Al Hilal Omdurman ili akili ya kila mmoja aielekeze kwenye mchezo huu, nimefurahi kwa namna wachezaji walivyojituma kwenye michezo mitatu mfululizo waliyocheza, miwili dhidi ya TP Mazembe na mmoja uliopita," kocha huyo alisema.
Yanga, iko nafasi ya tatu ya msimamo ikiwa na pointi saba, ambapo inahitaji ushindi pekee ili kufuzu, ambapo itafikisha pointi 10 na kuiacha MC Alger ikisalia na pointi nane.
MC Alger, ina pointi nane kwenye nafasi ya pili, ikihitaji sare ya aina yoyote ili kufuzu kwani ikifanikiwa itakuwa imefikisha pointi tisa, Yanga itaambulia pointi nane.
Wakati huo huo, klabu hiyo imetangaza kumsajili winga mpya, Ikangalombo kutoka AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo).
Klabu hiyo imemtangaza Mkongomani huyo muda mfupi kabla ya dirisha dogo la usajili halijafungwa.
Ikangalombo anakuwa mchezaji wa pili kutambulishwa na mabingwa hao watetezi baada ya beki wa pembeni, Israel Mwenda, aliyetua Jangwani akitokea Singida Black Stars.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED