Yanga: Ahsanteni, haikuwa riziki CAF

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:01 AM Jan 21 2025
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe
Picha:Mtandao
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe

KLABU ya Yanga imesema ilifanya kila kitu kuanzia kwenye uongozi, benchi la ufundi na wachezaji kuhakikisha wanafuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini haikuwa riziki yao kwa msimu huu.

Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, aliwataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa watulivu na wavumilivu kwa wanachopitia hivi sasa, kwani wanajipanga kwa ajili ya msimu ujao warudi na nguvu mpya, ikiwamo kufanya maboresho ya usajili kwenye dirisha kubwa.

Jumamosi iliyopita, Yanga ilihitimisha safari yake kwenye hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kulazimishwa suluhu dhidi ya MC Alger ya Algeria kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, matokeo ambayo hayakutosha kuifanya ifuzu hatua ya robo fainali, badala yake kumaliza Kundi A, ikiwa nafasi ya tatu, ikimaliza nafasi ya tatu, ikizipa nafasi MC Alger na Al Hilal Omdurman ya Sudan kusonga mbele.

"Haikuwa riziki. Hicho ndicho nachoweza kusema. Tumshukuru Mungu kwa sababu watu wote waliokwenda uwanjani, walikwenda kuona Yanga ikifuzu robo fainali, kilichotokea kila mtu ameona, si riziki, tutajipanga wakati ujao, nadhani tutafanya maboresho msimu ujao, kila ambacho tunaweza kufanya kilifanyika ili tufuzu jamaa walikuwa vizuri sana," alisema Kamwe.

Alisema kwa sasa kumekuwa na maoni mengi kutoka kwa wanachama, mashabiki na wadau wa soka kuhusu nini kilikosewa na nini kifanyike, akisema mawazo yote yamekusanywa na wanayafanyiwa kazi.

"Unapokuwa kiongozi unakusanya kila kitu, kwa wanaosema hatukujipanga vizuri sawa, wanaotushauri tumekusanya ushauri wao na tunaufanyia kazi, ila kwa sasa kazi tuliokuwa nayo ni  kukusanya makombe yetu, la Ligi Kuu na Kombe la FA, ili msimu ujao turudi tena kwa ngumu kubwa," alisema.

Uongozi uliwashukuru wanachama na mashabiki wote waliowaunga mkono kwa njia moja ama nyingine kufika hapo walipofika, pamoja na wale waliokuwa wakifika uwanjani, hususan kwenye mchezo wa mwisho Jumamosi iliyopita.

"Shukrani kwa wanachama na mashabiki wote wa Yanga waliofika Uwanja wa Mkapa, Jumamosi iliyopita. Uwapo wenu na sauti zenu zilikuwa na thamani kubwa sana. Kumepambazuka, ni siku mpya, ya jana yameshapita yatupasa kusahau. Kila huzuni tuliyonayo moyoni, tuigeuze kuwa hamasa ya kutupa morali ya kuupambania ubingwa wetu wa Ligi Kuu na Kombe la FA.

"Tuko katikati ya mapambano, yatupasa kujidhatiti kweli kweli kurudisha makombe yetu kabatini na hili ni muhimu kuliko vyote. Tusongeni mbele kama kaulimbiu inavyosema, daima mbele nyuma mwiko," alihitimisha Kamwe.