Simba, JKT Tanzania kazini Ligi Kuu Bara

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:32 AM Dec 24 2024
Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola
Picha: Mtandao
Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola

KAZI moja ya kuvuna pointi tatu muhimu ndio kitu pekee ambacho Wekundu wa Msimbazi wanakihitaji kuelekea mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya 'Maafande' wa JKT Tanzania itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Mechi hiyo ni ya kiporo kufuatia kikosi cha JKT Tanzania kupata ajali walipokuwa wanarejea nyumbani Dar es Salaam wakitokea Dodoma.

Akizungumza jijini jana, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, alisema wataingia uwanjani wakiwa na malengo ya kuendeleza kasi ya ushindi ili kujiimarisha katika msimamo wa ligi hiyo inayoelekea mwisho wa mzunguko wa kwanza.

Matola alisema wanawaonya wapinzani wao JKT Tanzania kutoingia dimbani kwa kuwadharau kwa sababu wao wameimarika na hawako tayari kuona wanapoteza pointi katika mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10:00 jioni.

Kiungo huyo wa zamani wa Simba ameweka wazi kikosi chao kitakuwa kinabadilika kiuchezaji kutokana na namna mpinzani wao atakavyocheza, hivyo kamwe JKT Tanzania wasiingie kwa kukariri mfumo wao.

Kocha huyo alisema lengo na mpango mkakati wa kubadilisha mfumo ni kutaka kuwavuruga wapinzani ili wasifahamu walichoelezwa na makocha wao.

"Tutaingia uwanjani tukiwa na lengo moja tu la kusaka ushindi, tutaingia na mpango mkakati wetu, lakini tutakuwa tunabadilika kadri wao watakavyokuwa wanabadilika na hii itawachanganya kwa sababu kile ambacho walikifanyia mazoezi jinsi ya kutuzuia, watakutaka na kitu tofauti," alisema Matola.

Hata hivyo alikiri kuwa mchezo utakuwa mgumu kutokana na aina ya mpinzani ambaye wanakwenda kukutana naye.

"Haitakuwa mechi rahisi, JKT Tanzania ni moja kati ya timu bora sana kwenye ligi hii, pamoja na walikuwa hawana matokeo mazuri lakini wamekuwa na kiwango kizuri uwanjani, wana wachezaji ambao wanaifahamu vizuri ligi yetu hapa," alisema nyota huyo wa zamani wa Super Sport ya Afrika Kusini.

Akizungumzia juu ya siku za karibuni timu yao kuruhusu mabao mepesi, alisema wamekaa na wachezaji pamoja na kulifanyia kazi suala hilo mazoezini na hawafikirii kuona litajitokeza tena.

"Ni kweli, tumekuwa tunapata matokeo mazuri, lakini tumekuwa tukiruhusu mabao, sisi kama benchi la ufundi hatufurahishwi mwenendo huo, tumekuwa tukilifanyia kazi, naamini kwenye mchezo huu halitojitokeza tena," aliongeza Matola.

Naye Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, alisema wamejiandaa vyema kuwakabili Simba, huku akiisifia timu hiyo na mwalimu wao, Fadlu Davids, wameifanya kuwa tishio katika ligi kwa sasa.

"Tumpe pongezi Kocha Fadlu kwa kuitengeneza timu nzuri, ina vijana wengi ambao ndiyo kwanza msimu huu wameingia katika kikosi, iko vizuri kwenye kila kitu, ikiwa na mpira, ikiwa haina, inakabia juu muda mwingi, mawinga hao ni balaa,  kwenye kona, faulo pia ni hatari kwa hiyo tunajua tunakwenda kukabiliana na hali hiyo.

Lakini ili uwe bora ni lazima ukutane na timu bora pia, hata mwalimu mzuri lazima ukutane na yule aliye zaidi yako, tulichojiandaa nacho sana ni vipi tucheze wakati tuna mpira na jinsi ya kucheza wakati hatuna mpira, tunajua tunakwenda kucheza na timu bora, unaona wanaweza kupata matokeo popote pale, wakicheza nyumbani hata ugenini, hivyo katika mchezo huu tunataka kuwa wa kwanza katika kila tukio ili tuwe na mchezo mzuri," kocha huyo alisema.

JKT Tanzania haijapata ushindi wala kufunga bao katika michezo mitatu mfululizo iliyocheza ya ligi hiyo.