Serengeti Boys vitani CECAFA

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 10:30 AM Dec 24 2024
Serengeti Boys
Picha: Mtandao
Serengeti Boys

TIMU ya Soka ya Taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), inakutana na Sudan Kusini katika mechi ya kusaka hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA U-17), itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Nakivubo jijini Kampala, Uganda.

Mashindano hayo ni maalumu kwa kupata wawakilishi wa CECAFA katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U-17), zitakazofanyika Machi, mwakani nchini Morocco.

Serengeti Boys ilimaliza hatua ya makundi ikiwa ya pili wakati Sudan Kusini iliongoza katika Kundi B.

Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Aggrey Morris, aliliambia gazeti hili wachezaji wake wako tayari kwa mchezo huo na wanaamini watafikia malengo.

Beki huyo wa zamani wa Taifa Stars na Azam FC, alisema wamejipanga kukutana na ushindani kwa sababu timu zote zilizoingia hatua ya nusu fainali zina wachezaji wenye viwango vizuri.

Mechi nyingine ya hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo itawakutanisha wenyeji Uganda dhidi ya Somalia.

Fainali ya mashindano hayo yanayosimamiwa na CECAFA itafanyika Jumamosi.