Raphinha 'aoga' matusi akiivusha Barca 16 Bora

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:57 AM Jan 23 2025
Raphinha
Picha: Mtandao
Raphinha

MSHINDI wa mechi, Raphinha amesema matusi ya Benfica yalizua mzozo uwanjani baada ya bao lake la dakika za lala salama kuipa Barcelona ushindi mnono wa magoli 5-4 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa kwenye Uwanja wa da Luz, Jumanne usiku.

Bao la Raphinha dakika ya 96 lilikuwa muhimu kwa Barca katika mchezo ulioshuhudia mvua kubwa ikinyesha huko jijini Lisbon, huku vurugu kubwa zikiibuka kwa wachezaji na Raphinha akimwagiwa matusi.

"Mimi ni mtu ninayemheshimu kila mtu," alisema Raphinha, ambaye aliwahi kuwachezea wapinzani wa Benfica, Sporting CP, akiwaambia waandishi wa habari baada ya mchezo huo. 

"Wakati natoka uwanjani watu walikuwa wakinitukana, nikarudisha matusi, najua sitakiwi, ilinikasirisha na wachezaji wa Benfica waliendelea kunitukana.

"Mimi ni mtu ambaye ninaheshima kwa anayeniheshimu, lakini sinyamaziki wakinitusi. Ni kawaida baada ya kumalizika kwa mechi kama hiyo."

Usiku ambao haukuweza kusahaulika ulikuwa umejaa matukio ya vurugu, huku Raphinha akisema yuko katika kiwango bora zaidi cha maisha yake ya soka baada ya kufunga mabao mawili huku Barca ikishinda mara sita mfululizo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo kufuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora.

Raphinha sasa amefikisha mabao nane kwenye michuano hiyo ya Ulaya msimu huu akiwa amepitwa tu na Robert Lewandowski aliyefunga mabao tisa na kufikisha jumla ya magoli 22 katika mashindano yote.

"Nadhani niko katika wakati bora zaidi wa uchezaji wangu, ndio," alisema mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil.

"Tulijua itakuwa ngumu hapa, tulijua jinsi walivyokuwa wazuri, haswa kucheza mbele ya mashabiki wao, wachezaji wao mmoja mmoja na kama timu, lakini cha muhimu ni kwamba tulijua kuweka umakini wetu wakati wote wa mchezo.

"Tulikuwa na mawazo tunaweza kubadilisha mchezo baada ya mapumziko, tukafunga bao la pili ili kurejea mchezoni na tukafanikiwa kufanya hivyo mwishoni. Hatukukata tamaa na tukaandika ushindi."

Benfica hapo awali ilitumia fursa ya makosa kadhaa ya Barca kuongoza 3-1 hadi mapumziko kwa hat trick ya Vangelis Pavlidis.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ugiriki alifunga bao la kwanza dakika ya pili na kukamilisha matatu ndani ya nusu saa baada ya Lewandowski kusawazisha kwa penalti.

"Ulikuwa mchezo wa kichaa," alisema Kocha wa Barca, Hansi Flick katika mkutano na waandishi wa habari. 

"Benfica walifanya vizuri sana hasa kipindi cha kwanza, lakini tulifanya makosa mengi. Hatukulinda vizuri.

"Ni muhimu tuzungumze juu ya hili. Wapinzani wanaofuata wataangalia mechi hii na lazima tuifanye vizuri zaidi. Tutafanya hivyo.

"Wakati wa mapumziko tulisema tunataka kubadilisha kitu; tunahitaji nafasi nzuri zaidi. Na tulisema tunataka kurejea."

"Jambo bora zaidi ni mawazo ya timu katika kipindi cha pili, wanajiamini kila wakati," Flick aliongeza. 

"Nilikuwa na furaha na pointi moja, lakini kwa tatu ni bora zaidi. Ilikuwa umaliziaji mzuri. Tunawekeza sana katika kipindi cha pili, tunatengeneza nafasi nyingi zaidi na tulistahili."

Ushindi huo unamaanisha Barca wamekata tiketi ya kuingia hatua ya 16 bora wakiwa na mchezo mkononi nyumbani dhidi ya Atalanta ya Italia wiki ijayo.

"Kufikia moja kwa moja hatua ya 16, hii itatusaidia sana kwa msimu uliosalia, nina uhakika asilimia 100 juu ya hilo," alisema Flick.