Ramovic: Wachezaji Yanga wananielewa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:32 AM Dec 24 2024
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic

BAADA ya timu yake kupata ushindi mnono, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema tayari wachezaji wake wameanza kumwelewa nini anataka na kuongeza pia wako vyema katika utimamu wa mwili unaowafanya watekeleze kwa usahihi kile anachowaagiza.

Yanga ilipata ushindi wa mabao 4-0 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Prisons na kufikisha pointi 33 na kuifanya ipande hadi nafasi ya pili kwenye msimamo, nyuma ya Simba yenye pointi 34 kibindoni.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mechi hiyo ya juzi, Ramovic, alisema ana furaha sana kwa sababu wachezaji wake wameanza kuelewa mfumo ambao amekuwa akiuingiza katika kikosi chake.

Ramovic alisema timu hiyo itaendelea kuimarika kwa sababu amefanikiwa kubadilisha mfumo wa timu na sasa mashabiki na wanachama wa timu hiyo watarajie furaha.

 "Nadhani wachezaji wangu sasa wameanza kunielewa nini nataka, nina furaha sana kwa sababu namna ambavyo tunafanya mazoezi ndivyo wanavyocheza uwanjani, kilichobaki nahitaji kuona ni mchezaji gani katika kikosi changu anajituma zaidi uwanjani," alisema Ramovic ambaye ameiongoza Yanga kushinda mchezo wa tatu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Aliongeza anafurahi kuona afya za nyota wake zimerejea vyema na wako tayari kucheza soka la ushindani.

"Wachezaji wangu pia wameanza kuwa na utimamu wa mwili, ukiwa fiti unakuwa na uwezo wa kutekeleza kile ambacho umeagizwa kukifanya uwanjani, kama huna hali inakuwa tofauti," Ramovic alisema.

Pia aliwapongeza wapinzani kwa kuonyesha mchezo mzuri, huku akisema bado ana kazi ya kufanya ili kuendelea kukiboresha kikosi chake.

Naye Kocha Msaidizi wa Prisons, Shaaban Mtupa, amesema idadi kubwa ya wachezaji ambao ni majeruhi katika kikosi chake inawavuruga na kusisitiza ni lazima waingie sokoni kwenye kipindi cha dirisha hili dogo la usajili.

"Changamoto kubwa kwetu tumekuwa na lundo la wachezaji majeruhi, kama kina Samson Mbangula, Jeremiah Juma, Jumanne El Fadhili, Salum Kimenya, Mussa Haji, Aboubakar Ngaliema, sasa tumeanza kuingiza vijana wengine bado si wazoefu inachukua muda, nafikiri inabidi turudi sokoni kutafuta wachezaji, dirisha dogo limefunguliwa inabidi tutafute wachezaji wa kuisaidia timu hii iende mbele. Tuna shida kwenye ulinzi, ushambuliaji na hata upande wa straika," alisema.

Kuhusu kichapo hicho, Mtupa alisema  hawakutegemea kupata matokeo hayo, huku akiongeza mabao mengi waliyoruhusu ni makosa ya wachezaji binafsi na si kitimu.

"Hatukutegemea matokeo haya, ukiangalia ni kama wachezaji wangu waliingia wakiwa na presha, ni hali ya kutojiamini, tukawa tunapoteza pasi zisizokuwa na sababu, ukikutana na timu yenye wachezaji makini, wenye uwezo ni lazima wakuadhibu.

Kipindi cha pili baada ya maelezo kwenye vyumba vya kuvalia, hali ilibadilika ikawa nzuri, lakini tukaruhusu tena bao moja kwa makosa binafsi ya mchezaji likawa la nne," alisema.

Ligi Kuu Bara inatarajia kuendelea tena leo kwa Simba kuwakaribisha JKT Tanzania huku Singida Black Stars ikiwaalika KenGold kutoka Mbeya. 

Mabingwa watetezi, Yanga wao watashuka dimbani kesho kucheza dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja na Jamhuri wakati keshokutwa Prisons itawaalika Pamba.