MKURUGENZI mpya wa Ufundi wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, Abdihamid Moallin, amesema ataifanya timu hiyo kuwa kubwa barani Afrika, lakini pia kuzalisha wachezaji wenye vipaji na 'kulisha' klabu nyingine duniani.
Moallin alitangaza kuachana na KMC FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kama Kocha Mkuu na kutua rasmi Jangwani mapema wiki hii.
Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kupewa nafasi hiyo, Moallin, alisema lengo lake kubwa ni kuzalisha wachezaji vijana wenye vipaji, kwa sababu yeye ni muumini mkubwa wa kutumia nyota chipukizi.
"Lengo ni kuendelea kusaidia kuijenga klabu hii kubwa kwa mwelekeo sahihi, nataka tuwekeze kwa vijana kufanya akademi yetu kuwa moja ya vitalu bora nchini na Afrika kama ilivyokuwa Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Tunataka kuzalisha wachezaji bora kwa ajili ya timu yetu ya kwanza na timu ya Taifa ya Tanzania kwa ujumla, lakini kulisha timu nyingine nje ya nchi ili wacheze mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika," alisema Moallin.
Bosi huyo mpya alisema mbali na kuzalisha wachezaji kwa ajili ya timu kubwa ya wanaume, lakini pia lengo lake ni kuiimarisha kikosi cha Yanga Princess ili iwe ni timu ya ushindani tofauti na ilivyo sasa.
"Tunataka pia kuimarisha pia timu yetu ya wanawake ili nayo ianze kuwania mataji, ili iwe moja ya timu bora Afrika, iliteke soka la Tanzania na kucheza mechi za kimataifa, hasa Ligi ya Mabingwa Afrika ya Wanawake," alisema mkurugenzi huyo wa ufundi.
Aliongeza amekuwa na furaha ya kujiunga na Yanga kwa sababu ametua kwenye klabu kubwa na yenye historia ya kubeba mataji.
"Nina furaha sana kuwa Yanga, ni timu kubwa Tanzania na Afrika, naahidi nitashirikiana na wenzangu wa benchi la ufundi ili kuifanya klabu hii iendelee kuwa tishio," Moallin aliongeza.
Alilisifia soka la Tanzania limekuwa kwa kasi na kuwafanya wachezaji wengi wa nje ya nchi 'kumiminika' kuja kucheza soka la kulipwa.
"Soka la hapa limepiga hatua kubwa sana, kila mtu anaitazama Ligi Kuu ya Tanzania, haishangazi kushika nafasi ya sita Afrika, kiasi imefanya wachezaji wengi wa nje wanatamani kuja kucheza soka nchini, nadhani hili inabidi Watanzania wajivunie," alieleza Moallin.
Yanga ilianza kumtangaza Mjerumani, Sead Ramovic, kuchukua mikoba ya Miguel Gamondi na Mustapha Kodro, akiajiriwa kama Kocha Msaidizi, nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Msenegal Moussa N'Daw.
Kwa sasa Yanga inajiandaa kuikaribisha Al Hilal kutoka Sudan katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa Novemba 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED