BODI ya Ligi Nchini (TPLB), imesema Ligi Kuu Tanzania Bara itaanza kwa mechi za 'viporo' za Simba na Yanga, kabla ya kuendelea na raundi ya 17, imeelezwa.
Ofisa Mtendaji mKuu wa TPLB, Almasi Kasongo, alisema, ligi hiyo itarejea kuanzia mapema Februari kwa mechi kati ya Tabora United dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi na Yanga kuikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
"Tumeshapokea taarifa rasmi CHAN haitakuwepo tena, ilikuwa ianze Februari Mosi hadi 28, lakini Kamati ya Utendaji ya CAF imepeleka mbele, tarehe maalum hawajataja, kwetu tumeipokea.
Tulisimamisha ligi kwa ajili ya Kombe la Mapinduzi pamoja na CHAN, Kombe la Mapinduzi limeisha na CHAN imepelekwa mbele, tafsiri yake ni lazima ligi irejee mapema. Mpango wa awali wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi ni kuanza tena mwezi wa pili," alisema Kasongo.
Aliongeza wakati ligi inasimama timu nyingi zilikuwa zimecheza michezo 16, kasoro timu nne (Simba, Yanga, Tabora United na Kagera Sugar), ambazo ndizo zilikuwa zimecheza michezo 15, hivyo kwanza ni lazima viporo hivyo vichezwe.
"Tuna viporo kwa klabu mbili kwa timu zilizokuwa zinashiriki Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, Simba na Yanga, ukitazama msimamo kuna timu zimecheza mechi 16, zenyewe zina michezo 15, nafikiri na Kagera Sugar pamoja na Tabora United, tafsiri yake tutaanza kwanza kucheza mechi hizo za viporo, ndipo ligi iendelee kwa michezo ya raundi ya 17," Kasongo alisisitiza.
Hata hivyo, alikumbushia klabu hizo pia hazijacheza mechi zao kwa Kombe la FA, hivyo kabla ya kucheza viporo vya ligi wanapaswa kwanza kukamilisha viporo vya michuano hiyo.
"Nadhani wataanza na Kombe la FA, na baada ya hapo watacheza michezo ya ligi, muda upo, kuanzia sasa mpaka mwanzoni mwa mwezi wa pili kuna kiasi cha wiki tatu, timu zitakuwa zimeshakusanyana kuanza mazoezi," aliongeza ofisa huyo.
Simba yenye pointi 40 ndio vinara wa ligi hiyo huku KenGold ya jijini, Mbeya inaburuza mkia katika msimamo ikiwa na pointi sita kibindoni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED