KMC yaita timu zinazotaka wachezaji kwa mkopo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:50 AM Dec 21 2024
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Khalid Chukuchuku.
Picha:Mtandao
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Khalid Chukuchuku.

KLABU ya KMC, imesema imekamilisha usajili wa kiungo mkabaji ambaye watamtangaza hivi karibuni kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii, ikitarajia pia kuongeza wachezaji wengine kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, na ikizikaribisha klabu zinazotaka wachezaji wao kwa mkopo.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Khalid Chukuchuku, alisema katika usajili ni lazima kuambatane na kuwatoa wachezaji, hivyo wanatarajia kuwatoa baadhi ya wachezaji kwenda klabu zingine kwa mkopo.

"Tumepokea ripoti fupi ya mwalimu kwa namna anavyohitaji kuwa na maboresho ya wachezaji kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, tunalifanyia kazi, tumeshafanya usajili wa mchezaji mmoja ambaye ni kiungo mkabaji, kwa sasa sitomtaja muda ukifika tutamtangaza kwenye kurasa rasmi za mtandao wa klabu yetu na yapo maingizo mengine ambayo tunatarajia kuongeza.

"Siku zote ukiongeza wachezaji basi ni lazima wengine waondoke, kuna ambao tunawapeleka sehemu nyingine kwa mkopo ili wapate muda wa kucheza zaidi, tunatarajia maombi kutoka klabu mbalimbali za Ligi Kuu au Championship zikihitaji wachezaji wetu, na tutawatangazia watakaoondoka," alisema Chukuchuku.

KMC imemaliza mechi zake 15 za mzunguko wa kwanza, ikiwa kwenye nafasi ya tisa, ikiwa na pointi 18 mpaka sasa.

Katika michezo hiyo 15, imeshinda mitano, sare tatu, ikipoteza mechi saba, ikifunga mabao 10 na kuruhusu 20 kwenye nyavu zake.

Wakati huo huo, kikosi cha timu hiyo kimerejea kambini jana Ijumaa kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili, utakaochezwa Desemba 29, mwaka huu, dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Chukuchuku alisema baada ya mchezo wao dhidi ya Pamba Jiji, Jumatatu iliyopita, Kocha Mkuu Kalimangonga Ongalla, alitoa mapumziko ya muda mfupi.

"Leo (jana), kikosi chetu kinatarajia kuingia kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya Coastal Union, tunaamini wana timu nzuri lakini tunakwenda kupambana kwa ajili ya kupata ushindi," alisema.