KenGold yajipanga 'utukutu' wa Morrison

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:12 AM Jan 05 2025
Kocha Mkuu wa KenGold, Omari Kapilima
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa KenGold, Omari Kapilima

KOCHA Mkuu wa KenGold, Omari Kapilima, amesema ameandaa programu maalum kwa mchezaji Bernard Morisson, ambaye amesaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo kwa miezi sita.

Alisema kabla ya kumsainisha walizungumza na nyota huyo na kumpa masharti ya timu hiyo ambapo ni kuona anawapa kitu cha maana ndani ya uwanja na si vinginevyo.

Kapilima alisema hayo kufuatia rekodi ya mchezaji huyo na matukio ya utovu wa nidhamu akiwa kwenye klabu za Yanga na Simba.

Kocha hiuyo alisema mbali na masharti ambayo yamo ndani ya mkataba, anadhani utukutu wake hautokuwa na athari yoyote kutokana na kuwa kwenye klabu yenye mazingira tofauti na klabu za Simba na Yanga.

"Tulishazungumza naye kumpa masharti yetu tukakubaliana naye, tunajua uwezo na uzoefu alionao utatupa kitu duru la pili kuona tunaondoka mkiani kwenye msimamo wa ligi.

Hayuko peke yake, wapo mastaa wengine kutoka Zambia na DR Congo na wengine ambao wamechezea timu kubwa hapa nchini kama Yondani, hivyo tunaenda kuanza upya ligi” alisema Kapilima.

Morrison aliyejizolea umaarufu mkubwa nchini kutokana na kipaji chake kikubwa cha soka, pamoja na aina yake ya maisha ya kujichanganya na mashabiki, aliingia nchini mwaka 2020 na kujiunga na Yanga akitokea DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, akaitumikia kwa miezi sita kabla ya kutimkia Simba alipokipiga kwa mwaka mmoja na nusu hadi 2022, aliporejea tena Yanga.

Hata hivyo hakukaa kwa muda mrefu akatimkia AS Rabat ya Morocco ambako aliitumikia kwa muda mfupi kabla ya kupata majeraha na kumaliza mkataba wa mwaka mmoja akiwa nje ya dimba.