HUKU akisifu ubora wa watani wao wa jadi katika mechi ya 'Derby ya Kariakoo' juzi, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amefichua mbinu ambayo huwa anaitumia dhidi ya Simba kuwa ni kuwashambulia pembeni hasa dakika 30 za mwisho, kwani mabeki wake mara nyingi huwa wanakuwa wameshachoka.
Akizungumza baada ya mechi ya watani wa jadi iliyochezwa juzi, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na Yanga kushinda bao 1-0, Gamondi alisema hata mpango wake wa kuwaingiza Clement Mzize na Kennedy Musonda, kipindi cha pili ulikuwa ni mkakati wa kwenda kushambulia kupitia pembeni kwani alijua tayari, Shomari Kapombe, beki wa kulia na Mohamed Hussein 'Tshabalala' wanakuwa wameshakuwa hoi kwa kuchoka."Kipindi cha pili niliwaingiza Mzize na Musonda, ili wakimbie kwenye nafasi za wazi, tunafahamu Simba wanashambulia sana kupitia mabeki wao wa pembeni na dakika 30 za mwisho huwa wanachoka na kuacha nafasi kila mechi. Huo ndio ulikuwa mpango wetu.
"Tulifahamu kama ilivyo kawaida, watashambulia sana dakika 15 mpaka 20 za mwanzo kisha sisi mpango wetu ni kipindi cha pili kucheza mchezo wetu tunaoufahamu na ulilipa ila nawapongeza Simba wana timu nzuri imeimarika kimbinu na hili ndio jambo zuri zaidi kupata mechi nzuri," alisema raia huyo wa Argentina.
Alimalizia kumpongea Kocha Fadlu kwa kuibadilisha Simba na kuonekana kuwa timu tishio, inayocheza kimkakati na maarifa na kwamba hilo ni jambo bora kwa soka la Tanzania.
Wakati Gamondi akisema hayo, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amelia na mwamuzi Ramadhani Kayoko kwa kuwanyima walau penalti moja katika matukio mawili ya wazi kwenye mchezo huo, kutokana na mabeki wa Yanga kuonekana kumfanyia madhambi Kibu Denis, wanavyotaka huku akionekana kulikalia kimya jambo hilo.
Fadlu alipinga kuwa Yanga ni bora kuliko wao, bali akasema wana uzoefu tu, hivyo anachoona ni kwenda kukiimarisha zaidi kikosi chake.
Kocha huyo mbali na kumtupia lawama mwamuzi akidai timu yake imenyimwa penalti za wazi, aliisifu timu yake kuwa inazidi kuimarika kupata muunganiko na uzoefu, akidai hicho tu ndicho wanachozidiwa na Yanga.
"Si kwamba Yanga ni bora kuliko sisi, bali wana uzoefu tu, tunapaswa kuimarisha kikosi chetu na tunafahamu dirisha dogo lipo jirani, hivyo tutapaswa kuboresha zaidi kikosi chetu kwa kuwa mbio za ubingwa bado zipo wazi," alisema.
Yanga ilipata bao pekee dakika nne kabla ya mchezo kumalizika likiwa la kujifunga kwa beki Kelvin Kijili katika harakati za kuokoa mpira uliopigwa na Maxi Nzengeli, baada ya kutemwa na kipa, Moussa Camara kutokana na faulo ya Clatous Chama.
Matokeo ya mchezo huo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 15 na kwenda mpaka nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu, chini ya Singida Black Stars yenye pointi 16.
Mabingwa hao watetezi wameweka rekodi ya kucheza michezo mitano, ikishinda yote, ikifikisha mabao tisa bila kuruhusu wavu wake kuguswa na kuendelea kutopoteza mechi.
Kipigo ilichokipata Simba ni cha kwanza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ikishuka hadi nafasi ya nne ya msimamo ikisalia na pointi 13.
Timu hizo zitashuka tena kesho dimbani, Simba ikicheza dhidi ya Prisons, Uwanja wa Sokoine, Mbeya, saa 10:00 jioni, Yanga ikiwa Uwanja wa Azam Copmlex, Dar es Salaam, saa 1:00 usiku dhidi ya JKT Tanzania.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED