Fadlu: Tutashambulia mwanzo, mwisho

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:05 AM Dec 14 2024
Baadhi ya wachezaji wa Simba.
Picha:Simba SC
Baadhi ya wachezaji wa Simba.

KOCHA Mkuu wa Simba Fadlu Davids, amesema kwenye mchezo wa kesho dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia, watacheza kwa kushambulia muda wote wa mchezo kwa kuwa hakuna kingine kinachotakiwa zaidi ya ushindi.

Akizungumza kuelekea kwenye mchezo huo wa raundi ya tatu, Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi dhidi ya timu hiyo ya Tunisia, kocha huyo alisema haijalishi watachezaje, kama watacheza soka safi au vinginevyo, lakini kinachotakiwa ni kupata ushindi kwenye mchezo huo kwa njia yoyote ili kuendeleza rekodi ya kuzoa pointi tatu nyumbani ambazo zinaweza kuwasaidia kuvuka hatua ya makundi na kwenda robo fainali.

"Tunachohitaji ni ushindi tu, haijalishi tumecheza vipi, tumecheza vizuri zaidi kuliko wenzetu CS Constantine Jumapili iliyopita tukiwa ugenini, lakini wenzetu walitumia makosa yetu madogo kutuadhibu na wakashinda mechi, na sisi tunataka kupata ushindi kwenye mchezo utakaochezwa nyumbani mbele ya mashabiki wetu ambao watakuja wengi kutushangilia," alisema Fadlu.

Alisema kwa mahesabu ambayo wameyapiga, wana uwezo wa kuliongoza Kundi A, au kushika nafasi ya pili nafasi ambazo zitawasaidia kusonga mbele.

"Tukishinda tutafikisha pointi sita, na tutakuwa tumebakisha michezo mitatu ambayo kwa vyovyote hatuwezi kucheza yote bila kupata pointi tatu au nne katika ya mechi hizo, na kimahesabu ukishakuwa na pointi tisa au kumi utakuwa umeshavuka kundi," alisema.

Kutokana na hilo, alisema katika mchezo wa kesho amewataka wachezaji wake kushambulia muda mwingi wa mchezo na kutumia kila nafasi itakayopatikana ili kupata mabao yatakayowawezesha kuzoa pointi tatu.

"Tunataji mabao, ikiwezekana mengi zaidi ambayo yanaweza kutusaidia mbele ya safari kama tutakuwa tumefungana pointi na wenzetu mwishoni mwa michezo ya kundi hili," alisema Fadlu raia wa Afrika Kusini.

Simba inashika nafasi ya tatu kwenye kundi hilo linaloongozwa na CS Constantine yenye pointi sita, Blavo do Maquis ya Angola ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu kama Simba iliyo chini kwa idadi ya mabao ya kufunga, huku CS Sfaxien ikiburuza mkia, ikiwa haina pointi yoyote.

Katika mchezo wa kwanza, Simba iliifunga Bravo do Maquis ya Angola bao 1-0, kabla ya Jumapili iliyopita kufungwa ugenini nchini Algeria mabao 2-1 dhidi ya CS Constantine.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema kama timu hiyo imefungwa na timu mbili zilizo kwenye kundi hilo, moja ikiwa nyumbani kwao, basi hakuna namna yoyote wao washindwe kupata pointi tatu kutoka kwao.

"Itakuwa haina maana yoyote, yaani timu imefungwa kwao, halafu imepoteza mechi nyingine ugenini inakuja kucheza na timu ambayo tunajinasibu kuwa tunataka kwenda robo fainali halafu tushindwe kuchukua pointi tatu itakuwa si sawa. Kama Simba tunaitaka robo ni lazima na sisi tuchukue pointi tatu kwao ," alisema Ahmed.