KIKOSI cha Azam FC kinatarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Manungu Complex ulioko Turiani mkoani, Morogoro.
Kwa sasa Mtibwa Sugar yenye pointi 35 ndio vinara wa Ligi ya Championship ikifuatiwa na Mbeya City yenye pointi 34 kibindoni, lakini imecheza mechi moja zaidi ya timu hiyo inayowania tiketi ya kurejea tena katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ofisa Habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe, alisema mechi hiyo imeandaliwa ili kukiweka sawa kikosi chao kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ibwe alisema kikosi chao kinaendelea vyema na mazoezi na kila mchezaji yuko tayari kuipambania timu hiyo ili kufikia malengo waliyoyaweka.
Hata hivyo Azam FC ilitolewa mapema katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na vigogo wa Ligi Kuu ya Rwanda, APR na sasa inapambana kuhakikisha inamaliza katika nafasi ya juu ili kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa hapo mwakani.
Wakati huo huo, uongozi wa Azam umempa mkataba mpya beki wao wa kati, Landry Zouzou ambao utamalizika ifikapo mwaka 2028.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam yenye pointi 36 iko katika nafasi ya tatu nyuma ya vinara Simba yenye pointi 40 na mabingwa watetezi, Yanga yenye pointi 39, hata hivyo imecheza mechi nmoja zaidi ya vigogo hao wa soka nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED