Wasomi wanavyomuunga mkono Rais wakihubiri nishati safi, ulinzi hifadhi

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 09:26 AM Sep 18 2024

Watalii ndani ya hifadhi ya misitu wa asili wa Kazimzumbwi.
PICHA: MTANDAO.
Watalii ndani ya hifadhi ya misitu wa asili wa Kazimzumbwi.

RAIS Samia Suluhu Hassan, anahamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia akiwa kinara mtetezi wa kuachana na upishi wa kuni, mkaa na samadi zinazoathiri afya.

Tafiti za matumizi ya nishati zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya Afrika inatumia nishati isiyo safi jikoni na kwa Tanzania ni asilimia 90 inatumia nishati isiyo chafu kupikia.

Rais Samia anasema mbali na vifo, nishati chafu inaathiri kimazingira, wanawake na mabinti hutumia muda mwingi kutafuta kuni na mkaa badala ya shughuli nyingine, hivyo anadhamiria kuwaondoa Watanzania katika changamoto hiyo.

Tanzania Landscapes Restoration Organization (TaLRO), ni taasisi inayoanzisha juhudi za kuunga mkono kazi za Rais Samia kulinda mazingira na kutumia nishati safi, kwenye hifadhi za misitu.  

Dk. Elikana Kalumanga, mshauri wa asasi hiyo, anazungumza na Nipashe, akifafanua jukumu hilo kuwa mradi unalenga mambo kadhaa mojawapo kupanda miti ya asili 10,000. 

Anataja hifadhi ya msitu wa Kazimzumbwi ulioko Kisarawe mkoa wa Pwani, ambao kwa miezi sita watapanda miti hiyo.

Aidha TaLRO kwa kushirikiana na NMB, itaimarisha uchumi wa wanajamii vikiwamo vikundi vya kuweka na kukopa wakiwahusisha wafuga kuku na nyuki.  

“Mradi utawashirikisha wanakijiji cha Maguruwe wilayani Kisarawe, kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia miradi midogo chini ya mfuko wa mazingira.

Dk. Kalumanga anasema: “Asasi hii ilianzishwa na vijana waliomaliza chuo kikuu mwaka 2019 wakishirikiana na walimu wao wakilenga kuondoa dhana ya kuwa wanapomaliza vyuo lazima wawe na uzoefu wa miaka kadhaa. Ukiangalia uzoefu anaupata wapi wakati ametoka kumaliza chuo?” 

Anasema wazo likaibuka kwamba walimu waanzishe taasisi ambayo itahifadhi mazingira, ili waliokuwa wanasoma wayafanye mazoezi na kazi kwa kujitolea lakini kwa ufanisi zaidi. 

Anasema waliamua ofisi iwe Kisarawe kwa sababu ni eneo lenye msitu wa asili wa Kazimzumbwi moja ya eneo lenye bayoanuwai nyingi duniani. 

“Ni kama misitu ya Usambara na Uluguru. Kazimzumbwi una eneo na visehemu yenye umuhimu na hadhi kama msitu wa Amazon,” anasema Dk. Elikana.

Anasema Kazimzumbwi ni miongoni mwa maeneo makubwa 25 duniani yenye umuhimu mkubwa wa bayoanuai. 

“Unapotaja maeneo manane Afrika yenye baioanuwai kubwa hiyo misitu inayoitwa (coastal east Africa), Kazimzumbwi ipo kwenye hayo maeneo na unaijumuisha kwenye maeneo hayo manane. 

Anasema kwa hiyo wakaona ni vyema akaonyesha utaalamu kwa kushirikiana na serikali na baadhi ya wadau wa mazingira kurudisha uhalisia kwa kupanda miti ya asili eneo hilo. 

Anaongeza kuwa hawapandi misitu isiyo ya asili na ikitokea labda miti ya matunda na mbao, itapandwa maeneo ya mwananchi mmoja mmoja kama nyumbani ili kuongeza kipato cha familia. 

MALENGO NA ELIMU 

Dk. Elikana anasema jamii lazima ielimishwe na kubadili dhana kuwa maeneo yaliyohifadhiwa ni kwa ajili ya Wakala wa Misitu (TFS) au Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA). 

“Mfano kwa siku Dar es Salaam inahitali lita milioni 500 za maji na DAWASA inachofanya ni kusambaza na si kuyazalisha yanatoka kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kutoka milima ya Uluguru. 

“Kila mmoja anapambana apate mboga za majani Dar es Salaam, lakini wakulima wa pembezoni wanategemea mito midogo inayopita pembeni na uhai wa hayo maji kwa Dar es Salaam yanatoka Kazimzumbwi.” Anakumbusha. 

Anafafanua zaidi kuwa vyanzo vingi vya maji Dar vinatokana na maeneo hayo kwa hiyo umuhimu wake mkubwa na si kwa ajili ya TFS au TANAPA.

Anakumbusha kuwa pakiharibika mfanyakazi wa TFS akiharibu atahamishiwa sehemu nyingine na kuendelea kupokea mshahara wake kama kawaida, lakini wana Dar es Salaam hasa Kisarawe, wataishi kwa taabu.

 Anasema utunzaji wa maeneo yenye misitu ya asili una uhusiano mkubwa na uchavushaji wa mazao na hata maua ya aina tofauti. 

“Ukiona mtu kazalisha mahindi  na kuvuna kuna viumbe wamehusika kuchavusha na sisi tunachukulia kawaida kuwapoteza hao viumbe. Tuwajali.”

 Anasema ukifika Ujerumani, Uholanzi, Uingereza na Canada wizara zao zinaagiza nyuki na vipepeo kwa ajili ya kuchavusha mazao akiwataka Watanzania kubadilika.

Anaeleza kuwa kwa nchi maskini ni gharama kubwa, lakini kinachoweza kusaidia ni kufanikisha kuzaliana viumbe hao katika misitu ya asili kwa jamii kushiriki kuhifadhi na kama haitashiriki ijue faida zake.

Mradi huo anasema unalenga kuwainua wanawake na vijana kwa kupatiwa elimu ya kutafuta fedha, kuweka na kukopa kutoka Benki ya NMB. 

“Tunashirikiana na Benki ya NMB Kisarawe tuanze kusaidia wananchi kuhusu elimu ya fedha na mikopo halafu waweze kupata mikopo nafuu na tuwasaidie kuanzisha shughuli za uhifadhi mfano miradi ya kuku, nyuki na utalii hasa kwa vijana wadogo waanze kuzifanya hasa Maguruwe, Kisarawe na vijiji vya Kazimzumbwi.” 

Anasema pia mradi utajielekeza kupitia hiyo misitu kutengeneza ‘living laboratory’ yenye data kamili, mfano mtoto anapoona kipepeo kinavyokua kuanzia funza anayemaliza mazao shambani hadi anakua kipepeo inatakiwa aelewe na aone mchakato. 

Mkazi wa kijiji hicho, Shaban Said, anasema anatarajia mradi huo utabadili maisha ya wanavijiji hasa kuondokana na matumizi ya  mkaa na kuni ambayo ni chanzo cha uharibifu wa mazingira. 

“Ulinzi wa misitu ya asili ni muhimu lakini mtu anakata miti maeneo ya hifadhi kutokana na kukosa elimu pia kwa sababu uchumi wake ni duni, atapikia nini? Hawezi kumudu gharama ya nishati mbadala kama gesi,” anasema. 

Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Msimbu, Huruma Jacob, anasema mradi huo utawaimairisha wananchi kimapato kwa kuwa utakuwa endelevu.

 Awali, akizindua mradi huo Katibu Tawala wa Wilaya ya Kisarawe, Bupe Mwakibete, anasema mradi huo unaunga mkono juhudi za serikali katika ulinzi wa mazingira ikiwamo kupanda miti.

 TaLRO, ni asasi ya kiraia inayofanya kazi za kuhifadhi maliasili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwamo jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa mfano misitu ya Kazimzumbwi.

 TaLRO inasisitiza kuwa uhifadhi endelevu unahitaji ushiriki wa jamii na zinufaike na faida za hifadhi, kama vile miradi ya jamii katika kukuza kipato cha kaya na cha mtu mmoja mmoja.