BARABARA ya kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ni mbovu, hali inayohatarisha afya za wagonjwa na watumiaji wengine wa barabara hiyo, pamoja na kusababisha vifo.
Barabara hiyo ipo chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Shinyanga, ikianzia Nguzonane hadi Mwawaza ilipo Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa.
Wananchi, wagonjwa, madaktari, madereva wa bajaji, na magari ya kubeba wagonjwa wamekuwa wakilalamikia ubovu wa barabara hiyo tangu hospitali ilipoanza kutoa huduma rasmi za matibabu mnamo Desemba 29, 2022.
Nipashe ilifanya uchunguzi na kuandika makala tatu zinazoelezea athari zitokanazo na ubovu wa barabara hiyo, ikionyesha ukubwa wa tatizo hilo.
Mnamo Januari 30 mwaka huu, TARURA Wilaya ya Shinyanga iliamua kufanya ukarabati wa muda wa barabara hiyo kwa kufukia mashimo ili kurahisisha usafiri wa wagonjwa wanaokwenda kupata matibabu, wakati wakisubiri fedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami.
Februari 10 mwaka huu, Ofisi ya Rais TAMISEMI ilitangaza zabuni kupitia gazeti la serikali Daily News, pamoja na kuweka taarifa hizo kwenye mfumo wa mtandaoni NeST ili kumpata mkandarasi wa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Zabuni hiyo inaonyesha kuwa maeneo yatakayojengwa kwa kiwango cha lami ni kutoka Nguzonane hadi Mwawaza ilipo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Aidha, barabara kutoka Swyinetone hadi Ndala itajengwa ili kuunganisha Kituo cha Afya Kambarage na barabara ya Mwawaza, jambo litakalorahisisha usafiri kwa wagonjwa wenye rufaa.
Katika zabuni hiyo pia imebainishwa kuwa Stendi Mpya ya Mabasi ya Katunda itajengwa, na kwamba ujenzi wa miradi yote hiyo utachukua muda wa miezi 15.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Shinyanga, Mhandisi Samson Pamhili, amesema baada ya zabuni hiyo kutangazwa, wanamsubiri mkandarasi apatikane ili ujenzi uanze mara moja. Amebainisha kuwa ujenzi wa miradi yote hiyo utagharimu shilingi bilioni 21, fedha zilizopatikana kutoka Benki ya Dunia.
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira, na Watu Wenye Ulemavu), ameishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio cha wananchi wa Shinyanga kuhusu ubovu wa barabara hiyo. Amesema kuwa suala hilo lilikuwa linamuumiza kichwa, lakini sasa tatizo linakwenda kutatuliwa.
"Wananchi wa Shinyanga waendelee kuiamini serikali yao. Nimepambana kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami, na sasa tumeshapata fedha kutoka Benki ya Dunia, hivyo utekelezaji unakwenda kuanza," amesema Katambi.
Aidha, amewataka wakandarasi wazawa kuchangamkia fursa hiyo, ambayo pia itatoa ajira nyingi kwa vijana.
Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Zamda Shabani, akizungumza Februari 7, 2025, katika kikao cha baraza la madiwani, naye alieleza kusikitishwa na ubovu wa barabara hiyo. Alisimulia kisa cha mama mjamzito aliyempeleka hospitalini kwa ajili ya kujifungua, lakini kutokana na mashimo barabarani, alilazimika kukaa badala ya kulala kwenye bajaji, huku akilalamikia maumivu makali.
Alisema kuwa baada ya kufika hospitalini, tayari mama huyo alikuwa ameshapoteza mtoto wake.
“Tunashukuru serikali kwa jitihada za kutatua tatizo la ubovu wa barabara ya kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Watu wengi wameumizwa na barabara hii,” alisema Zamda.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Luzila John, alisema kuwa baada ya zabuni hiyo kutangazwa, anaomba serikali iharakishe mchakato wa ujenzi wake ili kuondoa usumbufu kwa wagonjwa.
Alieleza kuwa alifikia hatua ya kukata tamaa juu ya ujenzi wa barabara hiyo kwa sababu amekuwa akiilalamikia kwa muda mrefu kwenye vikao vya maamuzi, ziara za viongozi wakuu, na hata kuandika maombi rasmi bila kuona utekelezaji. Hata hivyo, sasa ameanza kuwa na matumaini baada ya zabuni hiyo kutangazwa.
“Nakushukuru wewe mwandishi wa habari, umekuwa ukiandika habari nyingi kuhusu ubovu wa barabara hii ya hospitali, na nimesoma makala zako. Kweli nimeamini vyombo vya habari vina nguvu sana, na sasa tatizo letu linaenda kutatuliwa,” alisema Dk. Luzila.
Mwananchi Eugen Archald, mkazi wa Mwawaza alipo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, alisema wanafurahia kusikia kuwa zabuni ya ujenzi wa barabara hiyo imetangazwa, kwani kilikuwa kilio chao cha muda mrefu. Alisema wamekuwa wakishuhudia ajali nyingi zinazotokana na mashimo, hasa wakati wa mvua.
“Sisi wakazi wa eneo hili tumeshuhudia ajali nyingi na namna wagonjwa wanavyoteseka kupita hapa. Kipindi cha mvua hali huwa mbaya zaidi, lakini tunashukuru kusikia zabuni imetangazwa, na tuna imani mkandarasi atapatikana na barabara itajengwa kwa kiwango cha lami,” alisema Eugen.
Miongoni mwa madhara yaliyowahi kutokea kutokana na ubovu wa barabara hiyo, ni ajali iliyotokea Mei 9 mwaka jana ambapo pacha wawili, Kulwa na Dotto Mahenga, wakazi wa Kijiji cha Lyandu, walifariki dunia baada ya kugongwa na gari lililokuwa likikwepa mashimo.
Madhara mengine yanajumuisha ajali nyingi, uharibifu wa mali za watu ikiwemo bajaji, magari binafsi na yale ya kubeba wagonjwa, pamoja na wananchi kuingia gharama kubwa za matengenezo ya vyombo vyao vya usafiri.
Sera ya Afya ya mwaka 1990 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2007, kifungu namba 5(b), inazungumzia huduma bora za afya zinazowafikia wananchi wote kwa urahisi. Hivyo, ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utasaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Shinyanga.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED