MKIMBIZI MTOTO HADI JAJI RAIA… Kamhadaa baba aliyeukataa uanasheria, akampa ukweli miaka 30 yuko maarufu

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 09:52 AM Nov 22 2024
Jaji Tujilane Chizumila.
PICHA: CHRISTINA MWAKANGALE.
Jaji Tujilane Chizumila.

JAJI Tujilane Chizumila, ana simulizi tangu akiwa na umri wa miaka 12 akiwa mkimbizi. Ameishi Tanzania wakiwa ni wakimbizi pamoja na wazazi wake, kutoka nchini Malawi.

Leo hii ana umri miaka 71), anaisimulia Nipashe, jijini Dar es Salaam, kuhusu safari yake kutumishi masuala mbalimbali kama vile, jinsia, diplomasia na sheria. Ana uwezo wa kuzungumza lugha takribani nne; Kiingereza, Kiswahili, Kijerumani na Kichewa, na kukielewa vyema kiyao.

Mazungumzo maalum  ya mwandishi wa makala hii na Jaji Chizumila, wiki jijini, Dar es Salaam yalikuwa hivi:

Swali: Umetunga kitabu chako kichwa cha habari kinasema ‘From A Refugee Girl to A Judge: My Journey’ una maana gani kwa lugha rahisi?

Jibu: Nimemaanisha kwamba mimi nilikuwa mkimbizi mtoto ‘a child refugee’ kuanzia miaka 12.  Hapa Tanzania nilikuja na wazazi wangu, baba yangu alikuwa ni Mkuu wa Itifaki wa Kwanza wa Malawi, baada ya kuwa mwalimu ndipo akachaguliwa kwenda Umoja wa Mataifa (UN), New York, Marekani, kuwakilisha nchi yetu.

Lakini baada ya mwaka, kukatokea vurugu kati ya rais Dk. Banda (Kamuzu) na mawaziri wa wakati huo, kwa hiyo ikaathiri wote ambao walikuwa ndio marafiki zao waliosoma pamoja. 

Baba yangu akaitwa arudi, lakini alipigiwa simu na wenziwe kwamba asirudi, kwa sababu serikali ilikuwa imekwishandaa magari mawili, moja kutubeba na mama yangu na sisi kutupeleka kijijini na lingine kumpeleka baba kwenda kumfunga.

Kwa hiyo, akimbie! Baba akatuambia tunatoroka tunakuja Tanzania kuwa wakimbizi. Najivunia kwa serikali ya Tanzania na UNHCR, kwa kutupokea na mpaka leo nimekuwa Jaji ambaye kwa sasa ni miongoni mwa majaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (makao yake makuu jijini Arusha).

Swali: Uliwahi kuwa raia wa Tanzania, sasa ni raia wa Malawi, Je, imekuwaje?

Jibu: Niliwahi kuwa raia wa Tanzania, kwa sababu niliolewa na Mtanzania (tena Msukuma…(akionyesha kicheko kidogo). Niliolewa mwaka 1975 nina watoto wawili, baada ya miaka kadhaa tulitengana na nikaamua kurudi nyumbani na kurudisha uraia na kurudi Malawi.

Swali: Tukirudi katika ‘status’ yako kwenye ‘cv’ (wasifu) wako ulikuwa jaji na sifa zingine unazungumziaje, haki za binadamu mambo kisheria? Uliipenda hii kazi? 

Jibu: Wakati baba kuwa amekwenda UN sisi (watoto) tulibaki na mama (Malawi), tukamfuata baada ya miezi kadhaa tukafika New York. Mimi nilikulia sana kijijini kwa mama yangu. 

Kwa sababu miaka ya 1950 wakati mimi na wadogo zangu wanazaliwa, mimi nilikuwa wa kwanza na baba alikuwa anasoma Chuo Kikuu cha ‘Salisbury’ ambacho sasa ni Harare huko Zimbabwe,na baadaye akaendelea kwenda kusoma Lesotho na kisha Afrika Kusini.

Wakati huo ukumbuke tulikuwa chini ya ‘Federation’, Umoja wa Nyasaland, ambayo ni Malawi sasa hivi, Northern Rhodesia ambayo ni Zambia sasa na Southern Rhodesia ambayo ni Zimbabwe. Tulikuwa hatuna chuo kikuu, kwa hiyo ilibidi kupita huko.

Mwandishi wa Nipashe, alipozungumza na Jaji Tujilane Chizumila, hivi karibuini katika Uwanja wa Ndege, Julius Nyerere, Dar es Salaam. PICHA: MPIGAPICHA WETU.
Wakati baba anasoma alitupeleka nyumbani kwa mama yangu kwa babu na bibi mzaa mama. Babu alikuwa ni mwalimu wa shule ya msingi na mama. Nilikaa sana kijijini, baadae aliporudi kutoka masomoni tukahamia Zomba, ambao ulikuwa mji mkuu wa Malawi wakati huo, kabla ya kuhamishiwa Lilongwe.

Kwa hiyo, kuwa mtoto wa kukulia kijijini tumefika New York, unafungua macho unaiona, tulisoma tu kwenye jiografia, kumbe mamabo? yako hivi, ila ilikuwa ni mshangao mkubwa sana baba amekuja ‘airport’ (uwanja wa ndege) na dereva mzungu (walipowasili New York)… tukasema hee baba una dereva mzungu! 

Hivyo tukaenda ofisi kwake kupaona na jengo la UN lilinifurahisha sana kwa sababu limejengwa tofauti, kulinganisha na majengo mengineyo  ambayo yako tu kwa ‘square’(mraba).

Siku hizi kuna wabunifu tofauti, enzi hizo ilikuwa ujenzi mwingi ni ‘square’, ila lenyewe jengo la UN lilikuwa kama nusu mwezi mwonekano wake. 

Nikasimama pale nashangaa, nitafanya nini na mimi nije nifanye kazi kama wewe! Akasema (baba) soma sana. Nilipofika huku (Tanzania), nikaingia darasa la sita, nikisoma Shule ya Msingi Chang’ombe (iliko DUCE, Dar es Salaam) hadi la saba alafu nikasoma sekondari ya Asumpta, enzi hizo ikiwa na jina hilo na baadae ikaja kuitwa Weruweru hadi kidato cha nne.

 Baada ya kukaguliwa wakimbizi waliwachekecha, serikali iliwachukua ambao walikuwa na uwezo wa kufanya kazi, hivyo baba yangu alisema anaweza kufundisha, akapelekwa Old Moshi Sekondari, ndio maana nilisoma Asumpta Sekondari.

Nikaja Sekondari ya Jangwani (Dar es Salaam), hadi kidato cha sita na nikaingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM 1977), kwa shahada ya kwanza, nikichukua sheria za kimataifa na diplomasia, kwa sababu mawazo yalikuwa kufanya kazi UN.

Pia, shahada ya pili nikafanya Sheria ya Kimataifa ya Umma. Nilifanya kazi miaka 10 na Shirika la Sheria la Tanzania (Tanzania Legal Corporation) na niliporudi Malawi nikapewa kazi kama wakili wa serikali.

Ila nilikaa nyumbani kwa mwaka mzima kwanza nikisubiri ‘clearance’ (kuhalalishwa) na serikali kwa sababu nilikuwa mtoto wa mhujumu wa serikalini (dissident).

Kwa hiyo, nikaja kupata kazi Save the Children Federation US mwaka 1989-1990. Nilifurahi kufanya kazi huku kwa sababu tulizifikia jamii za chini kabisa na lengo langu lilikuwa kuihudumia jamii. Baada ya mwaka ndiyo nikaitwa kufanya kazi kama wakili wa serikali. 

Baadae nikapata kazi shirika la UNHCR, nikafurahi kwa sababu ilikuwa na mimi nawashughulikia wakimbizi kama mimi nilivyoshughulikiwa.

Nikafungua kampuni yangu la sheria, nikawa mwananke wa kwanza mwanasheria kufungua kampuni binafsi.

Halafu nikachaguliwa kuwa Balozi wa Malawi Zimbabwe na Southern Africa Development Corporation (SADC). 

Baada ya miaka minne, nikachaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, kisha nikapata nafasi kuwa ‘Ombudsman’ na kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo.

Swali: ‘Ombudsman’ ni nafasi gani hii kisheria kwa lugha rahisi?

Jibu: ‘Ombudsman’ ni mtu anayesimamia sheria ni mtu anayeshughulikia kesi za watumishi wa umma, ambao wana madai tofauti kama mishahara au waliostaafu hawajalipwa, ambao wanapata uhamisho kwa sababu tofauti au hakuna maelewano, kati ya mtumishi na bosi.

Unakuwa unasikiliza kesi, inakuwa kama mahakama na unaweza hata kumuita rais akaja mbele yako kuja kujieleza, hata mawaziri na wenye vyeo vikubwa. Kwa Tanzania nafasi hii iko ndani ya Tume ya Haki za Binadamu imekuwa kama idara.

Baada ya hiyo kazi niliyoifanya Malawi kwa miaka mitano nikastaafu, ila nikaona kama bado nina nguvu. 

===

Nikaona tangazo, kwa kazi ya Jaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, ilikuwa mwaka 2017 kwa hiyo nikatuma maombi nikapata na ukiomba ukipata kuna eneo unasimamia la Umoja wa AfriKa (African Union region). Mimi ninasimamia SADC (Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara) yote kama ‘female judge’ (Jaji wa kike).

Tuko majaji 11. Tunachaguliwa majaji wanawake na wanaume kwenye kanda Tano za Afrika. Kuna kanda ya kusini ambayo ni huo ukanda wa SADC, kuna Jaji wa kiume anayetoka Afrika Kusini na mimi kutoka Malawi.

Kuna Afrika Mashariki ambako ni jaji wa kutoka Tanzania wa kike, na sisi wenyewe huwa tunachagua rais wetu na makamu wa rais na tumemchagua jaji wa Tanzania kuwa rais wetu, halafu kuna jaji wa Uganda ambaye ni wa kiume, kisha kuna Afrika Magharibi, Kati na Kaskazini, jumla ni majaji 10, wanawake watano na wanaume watano.

Ila ulifanyika uamuzi maalaum kutoka Umoja wa Afrika (AU), mwaka 2017 ili kuwe usawa wa kijinsia katika hiyo mahakama, wakati huo tulikuwa wanawake wawili, mimi na wa kutoka Algeria. 

Ila kuna jaji mmoja huwa anachaguliwa kuongeza idadi ya majaji 10 na kuwa 11.

Ukichaguliwa kwenye mahakama hii unakuwa na mkataba wa miaka sita alafu unarudi na ukichaguliwa tena unakuwa na mkataba mwingine kwa awamu ya mwisho, hapa mimi SADC ilinichagua tena na niko katika muhula wa mwisho. 

Swali: Majukumu gani hasa mnayafanya kwenye Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu? 

Jibu: Majukumu tunayofanya sisi zaidi ni kuhusu haki za binadamu, iwe uraia, kikazi, mashamba yaaani chochote. Ila ili ufike kwenye mahakama yetu ni lazima umalize mahakama zote za nchini mwako, kwa sababu mahakama hii ndio kubwa kuliko zote barani Afrika, ukiona hujaridhika unakuja kwetu kwa suala la haki za binadamu.

Pia, tunafanya kazi na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu yenye makao huko Gambia. Kwenye Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, tunakutana mara nne kwa mwaka na makao makuu yako Arusha.

Swali: Je, ulipenda kusomea hiki unachokifanyia kazi hivi sasa?

Jibu: Kusema ukweli ilikuwa ni bahati mbaya sikupenda kusoma sheria na haikuwa kwenye wazo langu. Mimi baba amenilipia ada toka tulipofika Tanzania hadi chuo kikuu, kabla ya kupata ‘scholarship’ ila enzi zile wazee hawakuwa wanampa nafasi mtoto kujichagulia taaluma. 

Wakati najaza fomu ukiwa kidato cha sita unakuwa na machaguo matatu; chuo kikuu; ualimu na nyingine. Na hata chuo kikuu pia unachagua usome nini, baba yangu alikuwa ni profesa wa ualimu na historia pale chuo kikuu. 

Alitaka niwe mwalimu. Ila mimi sikupenda, baba mwalimu, mama mwalimu, babu mwalimu, mashangazi walimu! Nikasema mimi sitaki, nilikuwa napenda jiografia nikataka niwe na kazi katika uwanja wa ndege na kufuatilia ndege zinapotua na kabla ya kupaa.

Nikaomba nifanye kazi pale pale chuo kikuu, baada ya kumaliza kidato cha sita kwa sababu sikwenda ‘National Service’(JKT). Kuna siku wakati tukiwa ofisi tunachambua fomu zilizojazwa nikamwambia bosi wangu, mimi sikupenda kusoma fani hii lakini baba kanichagulia ‘education’ (ualimu) ila sikupenda. 

Na kila nikiweka katika mfumo inakuja chaguo la kwanza, nikamwambia nifanyaje, akasema jaza fomu tutaipitia fomu. Baadaye majibu kutoka nikachaguliwa kwenda sheria, hii ilitokana na mabadiliko niliyofanya awamu ya pili.

Nikawauliza rafiki zangu jamani katika sheria si hakuna hesabu wakasema ndio, kumbe walinidanganya, unapoanza tu kusoma unakutana na mambo mengi kama ‘bank statement’ usipoyajua utamteteaje mteja, kwa kweli nilikatishwa tamaa ila sikuacha kuendelea kusoma sheria.

Niliporudi nyumbani, baba akabaki anashangaa mbona wewe umechaguliwa chaguo la pili badala la kwanza? Nikamwambia sijui, kumbe nilibadilisha. Baadae imepita miaka 30 nikamwita nilivyokuwa Balozi Zimbabwe, nikaja kumwambia nilibadilisha sikutaka kuwa mwalimu, alicheka sana. Hii ndio hatua niliyopita hadi kuwa mwanasheria sasa.

Swali: Unaandika vitabu kuhusu maisha, una kitabu pia cha ‘A widow's perspective – a personal experince’ kwa nini?

==

Jibu: Nilitumia hiyo ‘personal experience’ yangu kuwaelimisha  wabunge ili wapitishe sheria yaku ‘stop  property grabbing’ ambayo  ilikuwa imeshakatiliwa kupitishwa  mara ya kwanza bungeni kwasababu ilikuwa na changamoto kadhaa.  Niliwahi kuuliza baadhi ya wanaume ambao ni wabunge mjane ni nani? Wakasema ni mke aliyefiwa na mume wake. Nikawaambia mwanamke yeyote anaweza kuwa mjane. 

Baba mmoja kainuka akasema mimi atayemuonea mjane mama yangu hatutaelewana, nikasema kumbe umenielewa. Mjane anaweza kuwa ni binti yako, mama, dada, shangazi. Baada ya muda mfupi sheria iliyowahusisha wajane ilirudishwa bungeni na ilirekebishwa bila upinzani wowote.

Swali: Kwenye kazi hii kuna changamoto yeyote unayokumbana nayo?

Jibu: Kwanza katika kazi hii ninayoifanya ni kutofahamika kwa mahakama hii, kuna wafanyakazi wachache, suala la kifedha. Na kutokuifahamu mahakama hii kunasababisha kuwapo kwa kesi chache hasa wanawake wanashindwa kuleta kesi.

Swali: Ulikuwa Balozi kwenye nchi ngapi?

Jibu: Nilikuwa Balozi wa Zimbabwe, pia wa SADC (Southern Africa Development Community), nchi zote za kusini mwa Afrika. 

Swali: Umewezaje kufika hapo ulipo sasa, ikizingatiwa kuna dhana tofauti kuhusu mwanamke na changamoto za kuzifikia ndoto zake?

Jibu: Nawashukuru wazazi wangu, linapokuja suala la kusoma hakukuwa na masihara. Na mama yangu ijapokuwa alikuwa mwalimu wa shule ya msingi alikuwa ananifundisha ‘English literature’ na vitabu vingi vilikuwepo nyumbani hata vitabu vya sheria, nikiwa na ‘home work’ yangu nampa ananisahihisha ananiambia hapa hapana rudia.

Baba pia tabia yake ilikuwa lazima uhakikishe umesoma magazeti ya siku hiyo, umesikiliza taarifa ya habari. Atakaa anakunywa chai, anawaita…anza wewe nipeni ‘brief’ (muhtasari) hapa nchini kuna nini na kimataifa? Anauliza shuleni mmesoma nini? Na vitabu alikuwa navyo vingi na hakukuwa na sababu ushindwe kusoma.

Kulikuwa na msukumo mkubwa kuhusu kusoma, lakini pili ni tabia walijitahidi kutuambia kwamba lazima ujiheshimu na ujitegemee akili yako. Ila nakumbuka darasa letu chuo kikuu wasichana tulikuwa sita na wanaume 40. Pia, serikali zetu siku hizi zinatupa hiyo nafasi.

Swali: Unazungumza lugha ngapi?

Jibu: Kwa kuzungumza kwa uhuru zaidi nitasema ni lugha tatu kiingereza, Kichewa, Kiswahili. Mimi ni myao wa Malawi. Na jina langu Tujilane ni la kiyao, linamaanisha ‘reconciliation’ (maridhiano). 

Kijerumani pia najua, kwa sababu nimesoma shahada ya pili kwahiyo lugha. Ukiwa huku kwenye mahakama hii lazima ujue lugha nyingine ya AU kwa hiyo kiingereza nakijua na sasa nasomea kifaransa. Kiswahili mwaka huu kimeingizwa katika AU kwa hiyo huwa tuna wakalimani ambao wanasaidia kukalimani.

Swali: Kazi hii unaona ina changamoto katika utekelezaji wa majukumu na maisha ya kawaida.

Jibu: Tulipokuwa darasani walimu walikuwa wanatuambia ukiwa mwanasheria usipande daladala, zamani tulikuwa na mabasi yanaitwa UDA, kwa sababu huwezi kujua ndugu wa yule uliyemhukumu anaweza akakuvamia. 

Kujilinda na kujitenga ni lazima. Na pia unajilinda na watu wasije wakakuona upo na mtu fulani wakasema kuna mazingira ya rushwa.