KENGELE ya wito wa kudumisha amani, umoja, maelewano na mapatano imepigwa na Kanisa Katoliki, ikihimiza na kukumbusha taifa kuthamini zawadi kuu ya uhai na kuendeleza mshikamano wa udugu wa Watanzania.
Jukumu kubwa ni la viongozi wa vyama vya siasa kutimiza wajibu ili kuliweka taifa pamoja ndani ya ramani ya kisiwa cha amani na utulivu na mhifadhi wa kila raia bila kujali kabila, dini itikadi wala mtizamo.
Kanisa kuwakutanisha wanasiasa na viongozi mbalimbali kutoka serikalini na upinzani , kuwe njia ya kufungua pazia na kuingia kwenye barabara itakayoiweka pamoja Tanzania Bara na Visiwani kabla na baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa na ule mkuu wa 2025.
Wito wa Kongamano la Ekaristi ni ‘udugu wa kuponya ulimwengu’ lakini uwe udugu kuiponya Tanzania , ukiwakumbusha pia viongozi wa kijamii, dini,wasomi wanataaluma wa kila aina na mashirika ya kiraia kuwa wadau wa kuhubiri umoja na amani ya taifa .
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, Katibu Mkuu wa chama hicho John Mnyika na Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi wanakutana na kutazamana ana kwa ana wakiwa kwenye kongamano hilo la tano la Ekaristi Takatifu katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ushirikiano huo uendelezwe kwa manufaa ya kila mmoja.
Wameitwa, wameitikia wito. Hawakupuuza bali walisimama mbele ya halaiki ya waamini wengine wakiwa pamoja kwenye ibada na mbele ya Mungu kuonesha utayari wa kushirikiana.
Uamuzi huo si mdogo wala si wa kupuuzwa tena si wa kubahatisha .Badala yake wamethibitisha kiapo chao katika dhima ya kusimamia ustawi wa maendeleo ya amani ,utulivu, kuthamini utu na upendo.
Hatua ya kukutanishwa kwao ni wito wa moja kwa moja katika kuonesha kutii mbele ya jamii inayowatazama wakiwa viongozi na wanaotegemewa na wananchi kuwaongoza katika njia inayonyooka na inayojali haki za wote.
Viongozi hao kukutana katika ibada moja,haitokani na nguvu au ujanja wao bali ni karama toka kwa Mungu, inayoelekeza wito wa kuwataka kuepusha aina zote na majanga yanayotishia hatma bora ya taifa.
Kongamano hilo liwakumbushe wanasiasa na raia kuwa kauli mbiu kama tunahitaji ‘ watu, ardhi, siasa safi, uongozi bora, maendeleo ya uchumi, ustawi wa demokrasia ,utawala wa sheria au kuenzi haki za binadamu ili tuendelee havitafikiwa ikiwa amani itapuuzwa , kuchezewa na kuachwa itoweke.
Popote duniani amani, utulivu na umoja vilipokosekana kilichotawala ni shari, kuporomoka maadili, chuki , kukosa maelewano, vita, kumwaga damu, uasi na vifo vinavyoondoa zawadi kuu ya uhai ambayo ni haki ya msingi ya binadamu.
Watanzania wakumbuke kuwa haipo nchi yoyote duniani iliyofuzu kama haikuenzi amani na umoja wa kitaifa, kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.
Tanzania iliyojenga na kudumisha umoja wake, udugu wa watu wake bila kutumia nguvu na ushawishi wa ukabila ,dini, rangi au ukanda, haipaswi ikubali ipoteze tunu ya mshikamano wake kwa sababu yoyote.
Kengele iliyopigwa kwenye kongamano la tano la Ekaristi Takatifu imewajumuisha wanasiasa kwa niaba ya vyama na wafuasi wao.Viongozi wa vyama vikuu CCM na CHADEMA wakisimama bega kwa bega mbele ya viongozi wa dini yote hiyo ikionesha njia ya muafaka.
Kusimama kwao kuwe mwanzo wa kuelekea katika maelewano thabiti na kutuma ujumbe utakaodumisha amani badala ya kutokea vurugu, chuki na hamaki na wakati mwingine habari za mauti.
Siku zote jazba, chuki, husuda na hamaki hazijajenga badala yake vitu hivyo vinadhoofisha hupoteza uhai na maisha ya watu, kuvuruga amani ,maelewano , maendeleo ya kisekta na kuwarudisha nyuma watu na taifa wakibakia masikini tena wanaosongwa na migawanyiko.
Historia siku zote ni mwalimu, Tanzania bila amani isingefanya lolote katika harakati za kujenga nchi, kupigania uhuru wake na kufanikisha ukombozi Kusini mwa Afrika na kuhifadhi wapigania uhuru wa kila pembe ya dunia .
Vyama kadhaa vya wapigania uhuru viliendeleza harakati zake katika ardhi ya Tanzania ili viweze kupigania uhuru, kutafuta haki ,usawa na umoja katika nchi zao na leo Msumbiji, Angola, Zimbabwe, Afrika Kusini ni huru.
Katika vipindi hivyo vyote Tanzania ilikabiliana na mitikisiko, misukosuko ya ndani na nje, shida,vita na Uganda, furaha na misiba lakini imeendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu kutokana na taifa kuwa na umoja , amani, utulivu na mshikamano wa kindugu.
Licha ya kuwepo taabu , dhiki na hata upungufu wa baadhi ya bidhaa na huduma muhimu za kufanikisha maisha, Watanzania walibaki wamoja katika nyakati zote hatimaye kupata ushindi wakishikamana hivyo hata sasa amani hiyo iendelezwe kwa juhudi zote.
Sauti na wito kutoka katika kongamano hilo ni sauti muhimu kusikilizwa . Ni ujumbe wa amani wala si utani au mzaha bali ni wazi viongozi wa vyama vya siasa wanatakiwa kukutanishwa pamoja mezani kujadili hatma ya nchi hasa kudumisha amani ushirikiano na umoja pia kudumisha demokrasia na uhuru ambavyo ni haki ya kila mmoja.
Viongozi wa dini wameonesha njia ya kujenga demokrasia na misingi ya utawala bora kwa vyama vya siasa kushindana kwa hoja pamoja na dhamana ya kusimamia kwa vitendo usalama wa raia, uhai wao na mali zao, kujenga uchumi na kujiepusha na sintofahamu zinazojitokeza na kutia doa historia ya taifa hilo linalotukuka kwa amani na kushikamana.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED