WAZAZI ambao watoto wanaugua ugonjwa wa kifafa, wamwangukia Rais Samia Suluhu Hassan, kuwapa kipaumbele cha matibabu yenye gharama nafuu, kwa kuwa kundi hilo linakumbana na changamoto hasa kulipia huduma za kutibiwa.
Glory Mrema (pichani), mkazi wa Dar es Salaam, miongoni mwa akinamama ambao watoto wao wanaugua ugonjwa huo, anasema baadhi yao wameacha kuwapeleka watoto kuhudhuria kliniki na kutopata dawa kwa zaidi ya miezi tisa.
Akinamama hao wameeleza hayo jana, kwenye kongamano la kitaifa lililiandaliwa Chama cha Wazazi Wenye Watoto wenye Kifafa Tanzania (UWAKITA), kwa kushirikiana na Idara ya Afya ya Akili Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.
“Nashindwa kumudu gharama hizo tangu bima ya watoto ilipositishwa na serikali. Ombi langu kwa serikali, watoto wanaoishi na hali ya kifafa tuwalipie hata bima ya Toto Afya Kadi, ili wahudhurie kliniki, ombi letu kwa Rais Samia.
"Kidonge kimoja kinauzwa Sh. 1,500 kwa bei ya rejareja. Mtoto wangu anapaswa kumeza vidonge vinne kila siku, yaani viwili asubuhi na viwili jioni, bado dawa ya usingizi ambayo kidonge kimoja kinauzwa Sh. 500. Kwa siku moja mgonjwa wa kifafa anatumia Sh. 6,500.
"Kilio changu kwa Rais wetu, Samia Suluhu Hassan atuangalie kwa jicho la pekee, watoto wanaoishi na kifafa usalama wao ni dawa na chakula," anasema Glory.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED