Watishia kutoshiriki uchaguzi wa mitaa

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 04:32 AM Nov 24 2024
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Picha:TAMISEMI
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

WANANCHI 1,500 wa vijiji vitatu vya Kihangaiko, Msata na Pongwemsumbula katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, mkoani Pwani, wametishia kutoshiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kutokana na kutolipwa fidia zao kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Wakizungumza juzi katika kijiji cha Kihangaiko wakati wa kujadili suala lao, walisema Juni, 2021, walielezwa na serikali kwamba wahame katika vijiji vyao kwa ajili ya kupisha kambi ya jeshi kufanyia mazoezi.

Walisema baada ya kuelezwa hivyo tathimini ilifanyika haraka na kuahidiwa kulipwa ndani ya miezi sita, lakini hadi sasa wamekuwa wakipigwa danadana bila mafanikio.

Mwenyeviti wa kijiji kimojawapo ambaye kipindi chake cha uongozi kimeisha ambaye aliomba jina lake lisitajwe, kwa kuwa yupo kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi, alisema tangu walipofanyiwa tathimini wananchi walizuiliwa kutofanya shughuli zozote ikiwamo kilimo na kutojenga nyumba mpya.

 Mwananchi mwingine ambaye naye aliomba asitajwe kwa kuhofia usalama wake, alisema kinachoshangaza baadhi ya vijiji ambavyo vilifanyiwa tathmini wananchi walilipwa, hali ambayo inawatia mashaka huenda kuna agenda ya siri katika suala hili.

“Suala hili tulishalifikisha kwa viongozi mbalimbali wa serikali wakiwamo wa kitaifa, lakini bado hakuna mafanikio na tumezuiliwa na jeshi hakuna kufanya chochote na ukionekana unalima au unajenga utapewa kipigo cha nguvu, " alisema mwananchi huyo.

Diwani wa Msata, Selestine Semiono, alikiri  kuwa wananchi wa vijiji hicho bado hawajalipwa fidia zao kutokana na changamoto ya mwingiliano wa maeneo wakati wa kufanya tathmini.

Alisema baada ya changamoto hiyo, maofisa ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze walifika katika vijiji hivyo kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi wa mwingiliano wa maeneo kati ya mwananchi na mwananchi.

Semiono alisema mchakato huo umefanyiwa kazi na sasa tathmini itafanyika upya kuanzia mwezi Desemba, 2024.

Semiono aliwaondoa wasiwasi wananchi hao kwamba  serikali itawafidia baada ya tathmini kufanyika mwakani. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Chalinze, Ramadhani Possi, akizungumza na Nipashe, alisema malipo ya fidia yalikuwa ya awamu mbili ambapo awamu ya kwanza wananchi walishalipwa Sh. bilioni 9.1.

Alisema awamu ya pili ambayo itahusisha wananchi wa vijiji vya Kihangaiko, Msata na Pongwemsumbula wamesilisha maombi ya kuomba fedha kwa Mdhamini Mkuu wa Serikali.

"Tulishawasilisha maombi ya kutoa fedha za malipo ya fidia kwa mtadhimini na fedha zikitoka tutawalipa wananchi ila siwezi kusema ni lini zitaletwa hizo fedha," alisema.