Wanaochangia ununuzi gari la Lissu wafikisha milioni 76/-

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 09:53 AM Jun 17 2024
i Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
Picha: Mtandao
i Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

MCHANGO wa fedha za kumnunulia gari Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, umefikia Sh. milioni 76.7 kati ya Sh. milioni 300 zinazohitajika kumnunulia gari kiongozi huyo.

Fedha hizo zimetolewa na wadau hao ndani ya siku 24 tangu kuanzishwa harambee hiyo, ikiwa wa wastani wa Sh. milioni 3.2 kwa siku.

Lissu alithibitisha kufikisha kiasi hicho cha fedha kupitia mtandao wake wa X siku tatu zilizopita, akihamasisha wafuasi wake kuendelea kumchangia ili lipatikane gari kwa ajili ya kuendelea na shughuli zake za siasa.

“Kwa upendo, wema na ukarimu wenu gari jipya litapatikana, hili (lililoshambuliwa kwa risasi mwaka 2027) itawekwa makumbusho ya mapambano ya kidemokrasia nchini kwetu na kazi ya ukombozi itaendelea,” aliandika Lissu.

Mei 17, mwaka huu, wafuasi wa mwanasiasa huyo wakiongozwa na mwanaharakati Maria Sarungi, waliazimia kumchangia Sh. milioni 300 mtaalamu huyo wa sheria anunue gari jipya ili lile la zamani ambalo lilishambuliwa kwa risasi, lihifadhiwe kwa ajili ya ukumbusho.

Mei 18 mwaka huu, Lissu alikabidhiwa gari lake aina ya Toyota Land Cruiser V8, VXR na Jeshi la Polisi jijini Dodoma, baada ya kupita miaka saba tangu aliposhambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana nyumbani kwake Area D, Septemba 7, 2017.

Baada ya kukabidhiwa gari hiyo, Lissu alieleza lengo lake la kulitengeneza ili aendelee kulitumia katika shughuli zake za kisiasa mpaka pale litakapochoka, jambo ambalo wafuasi wake walipinga na kusisitiza watamnunulia gari jipya ili hilo liwe ukumbusho juu ya kile kilichompata.

Ndani ya saa 48 tangu Maria aweke namba za malipo kwa ajili ya kukusanya fedha hizo kupitia mitandao ya kijamii ya X na Instagram, zilikusanywa Sh. milioni 15, jambo lililoonesha dhamira ya dhati ya wafuasi wa mwanasiasa huyo.

Katika ukurasa wake wa X, Maria anaendelea kuhamasisha wafuasi na wapenzi wa kiongozi huyo kuchanga ili kiasi hicho cha fedha kipatikane na gari linunuliwe kwa muda waliopanga.