Shekhe Ali Mbaraka: Msiwatishe watu swala ya alfajiri

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 01:10 PM Jun 17 2024
MWENYEKITI Mstaafu wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Taifa, Shekhe Ali Mbaraka .

MWENYEKITI Mstaafu wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Taifa, Shekhe Ali Mbaraka ametoa angalizo kwa watoa Adhana kwenye misikiti mbalimbali, hususan swala ya alfajiri kutowatisha watu kwa maneno makali, kama vile shuka na vitanda walivyolalia ni sanda na jeneza.

Amesema wakati wa swala wakati wakiwaita waumini kwenda msikitini kuswali, baadhi ya watoa Adhana alfajiri huwaambia watu kuwa waende kuswali na wasiendelee kulala kwani vitanda na nyumba walimolala ni kama makaburi na mashuka waliyojifunika ni kama sanda.

Sheikh Mbaraka amesema hayo leo akizungumza wakati wa Baraza la Eid Kitaifa katika Msikiti wa Mohamed VI Kinondoni mkoani Dar es Salaam.

Ameongeza kuwa hayo maneno ambayo hutolewa wakati wa Adhana kwenye swala ya alfajiri hayapo katika mafundisho bali ni watu tu wameyaongeza kwa utashi wao na maneno hayo huwatia hofu na kuwatisha watu.

Aidha Sheikh Mbaraka amesema, kwenye jamii kuna watu wa dini na madhehebu mbalimbali, hivyo wakisikia maneno hayo wanaweza kuwa na hofu.