RIPOTI MAALUM: Ndoto ya Mwalimu Nyerere yazimwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:17 AM Jun 17 2024
Mwonekano wa majengo ya kilichokuwa Kiwanda cha Zana za Kilimo UFI (Ubungo Farm Implements), yaliyopo upande wa kushoto mwa Kituo cha Mwendokasi Shekilango, barabara ya Morogoro. Kwa sasa ni kiwanda cha mabomba cha TSP  Limited (Tanzania Steel Pipe).
Picha: Mtandao
Mwonekano wa majengo ya kilichokuwa Kiwanda cha Zana za Kilimo UFI (Ubungo Farm Implements), yaliyopo upande wa kushoto mwa Kituo cha Mwendokasi Shekilango, barabara ya Morogoro. Kwa sasa ni kiwanda cha mabomba cha TSP Limited (Tanzania Steel Pipe).

NDOTO ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuhakikisha Tanzania inajitosheleza kwa zana za kilimo, imezimwa.

Kiwanda cha zana za kilimo alichojenga mwaka 1970, hivi sasa hakizalishi zana hizo, bali kinazalisha mabomba ya maji.

Mnamo Machi 4, 1970, serikali chini ya uongozi wa Rais Nyerere, ilianzisha kiwanda cha zana cha kilimo UFI (Ubungo Farm Implements) kilichoko Shekilango, wilayani Ubungo, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Cleopa Msuya, aliyekuwa Waziri wa Viwanda wakati huo, lengo la kujenga kiwanda hicho ni kuhakikisha zana za kilimo zinapatikana nchini kwa bei nafuu wakati wote pasi na vikwazo.

Msuya anasema uanzishaji wa kiwanda hicho ni utekelezaji wa sera za kuendeleza viwanda muhimu nchini ambazo ni silaha muhimu za kupiga vita umaskini kwa kupunguza kutegemea zana za kilimo kutoka nje ya Tanzania.

Zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo kuendesha maisha yao, huku sekta hiyo ikichangia asilimia 26.5 katika Pato la Taifa na asilimia 65 ya malighafi za viwanda nchini. Hii ni kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kilimo za mwaka 2023/24.

Sekta ya kilimo ikiwa tegemeo kwa maisha ya karibu robo tatu ya wananchi, kiwanda hicho cha kwanza cha zana za kilimo kujengwa nchini, hiki sasa hakizalishi tena zana za kilimo kwa ajili ya wananchi. Zana hizo zinaingizwa nchini na wafanyabiashara wanaozitoa China, India na kwingineko ughaibuni.

Wakati dhamira ya Mwalimu Nyerere na serikali yake ilikuwa wananchi wawe na uhakika wa kupata zana hizo nchini na kwa bei nafuu, wakulima waliozungumza na mwandishi wa habari hii wanasema zana hizo sasa zinauzwa bei ghali na wakati mwingine baadhi hazina ubora.

Ni hali inayofanya mazingira ya kilimo kwa wakulima wadogo ambao ndio wengi zaidi nchini kuwa magumu, hivyo kukinzana na dhamira ya Mwalimu Nyerere ya kuinua uchumi wa wananchi kupitia kilimo.   

Kamati ya Kufuatilia Mafao ya Wafanyakazi 508 wa UFI inasema kiwanda hicho kilikuwa maarufu kwa kutengeneza majembe ya mkono, mapanga, majembe ya kukokotwa na wanyama, makwanja na zana nyinginezo za kilimo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ally Killindo anasema kiwanda hicho kimepata mwekezaji mpya kutoka China, Tianjin Machinery Import and Export Group, ambaye hazalishi zana za kilimo, bali mabomba makubwa ya maji.

"Wakati kiwanda kinafanya kazi na hadi tunasimamishwa tulizalisha zana nyingi sana, maghala yalikuwa yamejaa.

"Ghafla wakaanza kusema hakuna masoko licha ya kwamba wafanyakazi tulikuwa tunayaona masoko ya zana hizo kwenye maeneo mengi nchini kwa kuwa kilimo kilitegemewa sana. 

"Hadi sasa wakulima wanahangaika kupata zana za kilimo kwa kuwa zinaagizwa nje na watu binafsi ambao hujipangia bei," anasema Killindo.

Katibu wake, Makamba Kigome anasema wameandika barua na kuwaisilisha kwa Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson wakiwa na malalamiko ya kutolipwa stahiki zao zaidi ya Sh. bilioni moja ambazo ni malimbikizo ya mishahara, likizo, nauli, kodi ya nyumba na mafao. Barua iliwasilishwa ofisini kwa Spika Februari 14 mwaka huu.

"Tumeitumikia nchi yetu kwa juhudi, maarifa na weledi wa hali ya juu na kuiwezesha serikali kupiga hatua katika sekta ya kilimo. Tuliendelea kufanya kazi hadi Julai 31, 1998, serikali ilipokabidhi kiwanda kwa kampuni ya China ya Tianjin Machinery Import & Export Group kwa njia ya ubinafsishaji," inasomeka sehemu ya barua hiyo ambayo mwandishi ameona nakala yake. 

Katibu Killindo, aliyekuwa mfanyakazi wa UFI, anasema kiwanda kilizalisha zana zote muhimu za kilimo ambazo ni pamoja na majembe, mashoka, mapanga, plau, jembe palizi, jembe la matuta, na jembe la kupandia, kikiwa na matawi mjini Musoma na Mbeya.

Kwa ufupi, Killindo anasema aina 28 za zana kilimo zilitengenezwa na UFI, zikijumuisha pia visu vya kuvunia, haro, sululu, ndimi za plau, kabali, makwanja, beleshi, rato, koleo, minyororo, plau ya ardhi tifutifu, plau la kugawa matuta, mipini, plau la kupandia, mikasi, mashine za kupukuchulia, mikasi ya kuchongea, makoa na vifaa vyake, reki, nyundo, uzio na teso.

Mwandishi wa habari hii amebaini kuwa mashine zote zilizokuwa zinatumika kutengeneza zana za kilimo katika kiwanda hicho zimeng’olewa na hakuna taarifa rasmi juu ya zilikopelekwa.

Vilevile, mwandishi pia anafahamu kwamba kiwanda hicho kilijengwa kwa msaada wa Serikali ya China kutokana na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na nchi hiyo.

Hata hivyo, mkataba baina ya pande zote mbili haukuwahi kuwa wazi; Julai 1998 Serikali ya Tanzania ilikabidhi kiwanda kwa kampuni ya China ya Tianjin Machinery Import & Export Group kwa ajili ya ubinafsishaji. 

Mwandishi amebaini kuwa ubinafsishaji ulifanywa kwa matarajio ya kuboresha uzalishaji na kuingiza teknolojia mpya ya zana za kilimo.

Hata hivyo, imebainika kuwa mwekezaji mpya kutoka China, baada ya kukabidhiwa kiwanda, aliendelea kutengeneza zana za kilimo kwa muda mfupi kisha akageukia utengenezaji mabomba ya maji huku sehemu kubwa ya majengo ya UFI ikigeuzwa kuwa ghala la bidhaa kutoka China. 

Mwandishi anafahamu kuwa kwa hivi sasa kiwanda hakitengenezi tena zana za kilimo, bali kinazalisha mabomba kwa ajili ya miradi ya maji.

Mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda cha mabomba ya maji (jina tunalo) anasema, "baada ya kiwanda kubinafsishwa, baadhi yetu tulibaki hapa (kiwandani). Mwekezaji aliyechukua hakuendelea na uzalishaji zana za kilimo, anazalisha mabomba ya maji.

"Wengi wetu tupo hapa tangu mwaka 2009. Kiwanda kilianza uzalishaji mabomba mwaka 2016. Mwekezaji mpya alipoingia, aliondoa mfumo wa mashine za majembe na kufunga mfumo wa mabomba na baadhi ya mashine zilibaki zikaendelea kutumika, zikiwamo za kuchonga vipuri.

"Mwekezaji alianza kuendesha kiwanda kwa kuzalisha mabomba, wakati huo ilikuwa ni kwa ajili ya mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kuyapeleka Shinyanga. 

"Wakati kiwanda cha UFI kinafanya kazi, Watanzania ndio tulifanya kazi, hata kwenye masoko kama Kariakoo tulikuwa na maduka ya kuuza zana za kilimo, tulifurahi kupata riziki. Cha kushangaza ni kuwa licha ya kufanya kazi kwa miaka 20, niliambulia Sh. 600,000 tu," anadai.

Mwandishi alimtafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, kutaka kujua sababu za kiwanda kutozalisha tena zana za kilimo, hasara iliyopata serikali kutokana na kiwanda kubadilishwa matumizi na uwabikaji wa waliochangia kiwanda kutotekeleza jukumu lake la msingi.  

Hata hivyo, Juni 2 mwaka huu, Waziri Mkumbo aliahidi kujibu maswali hayo baadaye, lakini akitanguliza maelezo ya awali kwamba kiwanda hicho kilishafungwa. Hadi sasa hakuna maelezo zaidi ya waziri huyo juu ya kiwanda hicho.

*Itaendelea kesho