Polisi yaendelea kumsaka muuguzi aliyetoweka

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 07:55 AM Oct 05 2024
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Mwandamizi Msaidizi (SACP), Simon Maigwa
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Mwandamizi Msaidizi (SACP), Simon Maigwa

MAKACHERO wa Jeshi la Polisi, mkoani Kilimanjaro, bado wanahaha kumsaka Muuguzi wa Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Lenga Masunga (38), aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha Julai 2, mwaka huu.

Jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Mwandamizi Msaidizi (SACP), Simon Maigwa, aliiambia Nipashe katika mahojiano maalum kuwa, hadi sasa simu  za mkononi za Masunga, hazipatikani. 

Alisema katika uchunguzi wao walipofanya upekuzi nyumbani kwake, waligundua vyeti nyake vya elimu havikuwapo. 

"Ni kweli tunaendelea na uchunguzi lakini kikubwa kama kuna mwenye taarifa zake ni ruksa kupokea lakini mpaka sasa bado hatujabaini yuko wapi. 

“Kwa hali ilivyo mazingira yake bado hatujampata kwa sababu aliondoka na simu zake na vyeti vyake, hatujawahi kupata taarifa zake kwamba alipata kazi sehemu nyingine, kama tungepata simu yake inasomeka wapi ingekuwa ni rahisi kusema chochote, kwasababu wakati wa ukaguzi tulikuta vyeti vyake havipo," alisema. 

Masunga alikuwa muuguzi wa idara ya masikio, pua na koo (ENT). 

Inaelezwa kuwa Masunga alitoweka katika mazingira ya kutatanisha Julai 2, mwaka huu, nyumbani kwake, Mtaa wa Rau Pangaleni, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro alikokuwa akiishi. 

Wakati Masunga anatoweka alikuwa mapumziko ya siku mbili, kati ya Julai 2 na 3, mwaka huu.