Huduma za kipolisi zasogezwa zaidi Chemba

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:52 AM Oct 05 2024
Waziri Masauni akizungumza na wananchi baada ya kuzingua jiwe la msingi katika ujenzi wa kituo cha polisi Chemba.
Picha:Wizara Mambo ya Ndani
Waziri Masauni akizungumza na wananchi baada ya kuzingua jiwe la msingi katika ujenzi wa kituo cha polisi Chemba.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha polisi cha Daraja B Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma kunakwenda kusogeza huduma za kipolisi karibu zaidi na wananchi wa eneo hilo.

Waziri Masauni ameyasema hayo wilayani Chemba wakati akiweka jiwe la msingi  la ujenzi wa kituo hicho cha kipolisi ambacho utekelezaji wake umegharimu Sh. Milion 350 mpaka kukamilika kwake na kwamba kwa sasa upo katika hatua za mwisho.

Amesema dhamira ya serikali ni kulisogeza Jeshi la Polisi karibu zaidi na wananchi kupitia sera ya Polisi Jamii na ndio maana kuna askari wa cheo cha nyota moja katika kata zote nchi nzima.

"Serikali ya awamu ya sita inafanya maboresho ya mazingira ya kufanyia kazi Askari wa Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vipya na vyakisasa na vitendea kazi stahiki kwa askari," amesema Mhandisi Masauni.

Wakati huo huo, amelitaka Jeshi la Polisi kuendana na maboresho hayo yanayofanywa na serikali kwa utendaji kazi mzuri unaozingatia weledi na maadili ya kazi zao ili kuakisi jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kutatua kero za wananchi.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Masauni  amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Pahi, Wilaya ya Kondoa ambako amefanya harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo cha polisi kata na kufanikisha kupata kiasi cha Sh Milioni 18.4, ambayo itawezesha ujenzi kuanza Novemba mwaka huu.

Mhandisi Masauni yupo kwenye ziara ya kikazi Mkoa wa Dodoma, ambako pia ametembelea na kuunga mkono jitihada za wananchi katika ujenzi wa Shule ya  Sekondari Mnenia, Kondoa na kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba za walimu katika shule ya Sekondari Bolisa, Halmashauri ya Kondoa Mjini.