Mfumo stakabadhi ghalani wanufaisha wakulima

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 07:44 AM Oct 05 2024
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego
Picha:Mtandao
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego

MFUMO wa stakabadhi ghalani umeleta manufaa makubwa kwa wakulima wa dengu mkoani Singida na kwa kipindi cha miezi miwili, zaidi ya Sh. bilioni 25 zimezunguka kwa wakulima waliouza zao hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, aliyasema hayo juzi kwenye kikao cha kufanya tathmini ya utekelezaji wa mfumo huo katika msimu huu wa kilimo. 

"Singida tumetekeleza kwa mafanikio makubwa kwa muda mfupi wa miezi miwili hadi mitatu zaidi ya Sh. bilioni 25 zimezunguka kwa wakulima, hivyo tuna kila sababu ya kuipongeza serikali kwa kuweka mifumo rahisi ya wakulima wa nchi hii kupata stahiki zao zinazostahili," alisema. 

Dendego alisema mkoa wa Singida hautarudi nyuma katika kuuza mazao kwa kutumia mfumo huo licha ya kuwapo na kero mbalimbali. 

Alisema kwa mabilioni yaliyopatikana kwa wakulima kutokana na kuuza Dengu hakuna sababu ya kuuita mkoa huu ni maskini bali imejionyesha kuwa fedha zipo ila zilikuwa hazijaratibiwa vizuri. 

"Nani leo alitegemea dengu italeta Sh. bilioni 30 hapa? Ilikuwa  inauzwa lakini kwa sababu ilikuwa hairatibiwi vizuri ndiyo maana ilikuwa haionekani kama Singida inazalisha dengu kwa wingi," alisema. 

Dendego alisema iwapo mfumo huo utatekelezwa katika mazao mengine kama pamba, tumbaku, vitunguu, alizeti na mahindi, hakutakuwa na umaskini Singida. 

"Kwa hiyo Singida lazima safari hii tupindue meza na safari imeanza. Lazima  tushirikiane  na maafisa ushirika kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya. Mwelewe kipenga kimelia zile chengachenga mimi sizitaki. Tukisimama  wote hakuna atakayetushinda. 

“Mtu yeyote atayetaka kukwamisha utaratibu wa uuzaji mazao kwa kutumia mfumo huo atashughulikiwa kwa kuwa lengo la serikali ni kila mtu apate haki yake kulingana na jasho lake. 

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga, aliwataka maofisa ushirika kutoa elimu kwa wananchi ili kuufahamu mfumo huo. 

Dk. Mganga alitaka suala la usimamizi wa fedha zinazotokana na mfumo huo liwekewe utaratibu mzuri ili kuepusha malalamiko ya wakulima hasa wanapocheleweshewa malipo. 

Septemba 7, mwaka huu, wafanyabiashara wa mazao na makuli wa mizigo mjini Singida waliandamana na kufunga barabara kuu ya Dodoma-Singida-Shinyanga kwa magogo na miti wakipinga mfumo huo. 

 Mkoa wa Singida ulizindua rasmi utekelezaji wa mfumo huo kwa msimu 2024/25 kufuatia maagizo yaliyotolewa na serikali kupitia mwongozo wa biashara ya zao la dengu, mbaazi na ufuta. 

Mwongozo huo ulitolewa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA),Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC),Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) na Soko la Bidhaa (TMX).