Operesheni michezo kubahatisha, mfumo malalamiko ya kodi zaja

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 08:44 AM Jun 05 2024
Mchezo wa kubahatisha.
Picha: Mtandao
Mchezo wa kubahatisha.

SERIKALI imetamka itakamilisha katika mwaka ujao wa fedha mfumo wa kukusanya na kuchakata malalamiko ya walipakodi, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema.

Sambamba na hilo, imesema zitafanyika operesheni maalum nne dhidi ya michezo haramu ya kubahatisha, huku yenyewe ikiendelea kusaka Sh. trilioni 44.19 za kutekeleza mpango na bajeti ya serikali ambazo hivi sasa hainazo.

Waziri Dk. Mwigulu aliyasema hayo bungeni jana alipowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2024/25, akiomba Bunge kuidhinisha Sh. trilioni 18.287, huku akigusia ajenda nyingine ya 'vita' maalum kukabili ubabaishaji katika ununuzi serikalini.

Alisema vipaumbele vya mafungu ya wizara ni pamoja na kutafuta na kukusanya mapato ya Sh. trilioni 44.19 kati ya maoteo ya Sh. trilioni 49. 35 kwa ajili ya utekelezaji mpango na bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha.

Waziri huyo alitaja kipaumbele kingine ni kuimarisha na kusimamia mifumo ya mapato, matumizi na mali za serikali ikiwamo IDRAS, TANCIS, MUSE, NeST, CBMS na GAMIS, pia kuhudumia deni la serikali kwa wakati na kuboresha kanzidata ya kutunza taarifa za deni.

Dk. Mwigulu alisema wizara pia itatoa elimu ya huduma za fedha kwa wananchi kwa lengo la kukuza huduma jumuishi za fedha nchini na kujenga uwezo kwa wakaguzi wa ndani, kamati za ukaguzi pamoja na waratibu wa usimamizi wa vihatarishi katika taasisi za umma.

Alisema Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) kwa mwaka 2024/25 itafanya ukaguzi wa mapato na matumizi ya rasilimali za umma kama yalivyoidhinishwa na Bunge mwaka 2023/24.

"Ofisi itafanya ukaguzi wa kiufundi, ufanisi, miradi ya maendeleo na mifumo ya TEHAMA, ukaguzi maalum na kiuchunguzi kulingana na mahitaji, kuendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kujenga na kukarabati ofisi za mikoa na kuzijengea uwezo kamati za kudumu za Bunge za usimamizi na za kisekta ili kuzielewa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kuhusu vipaumbele vya taasisi za wizara kwa mwaka 2024/25, waziri huyo alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya jumla ya Sh. trilioni 29.42. Kati yake, Sh. trilioni 28.87 ni mapato ya kodi na Sh. bilioni 541.10 ni mapato yasiyo ya kodi. 

Alisema mamlaka pia itaendelea kutekeleza mkakati wa kudhibiti biashara za magendo ili kupunguza mianya ya upotevu wa mapato ya serikali.

Alisema Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu inatarajia kusajili wahasibu na wakaguzi wa hesabu 300 katika ngazi mbalimbali za uanachama.

Waziri Mwigulu alisema katika mwaka ujao wa fedha watatekeleza operesheni nne za kutokomeza michezo haramu ya kubahatisha, kukusanya mapato yatokanayo na michezo ya kubahatisha ya jumla ya Sh. bilioni 24.89, kuendelea kuelimisha jamii juu ya athari hasi za michezo ya kubahatisha na kusimamia uendeshaji Bahati Nasibu ya Taifa.

Ili kutekeleza majukumu hayo, aliomba Bunge kuidhinisha Sh. trilioni 18.17 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo ya wizara hiyo. 

Kati ya fedha hizo, Deni la Serikali ni Sh. trilioni 13.132, Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Sh. bilioni 14.276, Tume ya Pamoja ya Fedha Sh. bilioni 6.006, Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu Sh. bilioni 3.768, Hazina Sh. trilioni 2.130, Huduma za Mfuko Mkuu Sh. trilioni 2.629, Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali Sh. bilioni 69.655, Wizara ya Fedha Sh. bilioni 188.486 na NAOT Sh. bilioni 112.729.

*SOMA SEHEMU YA HOTUBA YA WAZIRI MWIGULU KUPITIA www.epaper.ippmedia.com