MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amewataka waandishi wa habari nchini kutumia kalamu na kamera zao kuilinda Tanzania ili iendelee kuwa na amani, utulivu na maendeleo.
Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, aliyasema hayo jana jijini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa Ofisi na aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba.
Alisema waandishi ni mhimili wa nne usio rasmi lakini wenye nguvu kubwa, ukitaka kukutikisa unatikisika na ukitaka kutuliza unakutuliza hivyo, waandishi wachague kutuliza nchi kwa kuwa inahitaji utulivu.
“Hii ni nchi yetu sote na sisi wote ni watanzania, nyinyi waandishi wenzangu wa habari ni watanzania na mnaishi Tanzania, hata kama kuna mwandishi wa habari sio mtanzania lakini anaishi Tanzania, wote tunajukumu la kuilinda Tanzania.
“Kazi yetu sisi waandishi wa habari ni kuilinda Tanzania kwa kalamu zetu, naomba kalamu zetu zitumike kuilinda nchi yetu, nchi yetu inataka amani, maendeleo, utulivu na haijazoea zogo wala vurugu tumkatae kwa nguvu zetu zote kwa kalamu zetu na kamera zetu yeyote anayetaka kutuvurugia tunu za taifa,” alisema.
Alisema baada ya sikukuu za mwisho wa mwaka atakutana na waandishi kwa ajili ya mazungumzo ili kuweka mikakati ya utendaji kazi.
Hata hivyo, alisema Desemba 19, mwaka huu, atatoa taarifa ya kwanza ya Msemaji Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.
“Utamaduni wa taarifa za Msemaji Mkuu wa Serikali ni muhimu sana, kuna mwingine anaweza kuchukulia poa, lakini niwaambie watanzania wakisikia msemaji mkuu wa serikali anazungumza wanasikiliza kwa sababu wanapata taarifa muhimu za serikali,” alisema.
Balozi Makoba alisema ameondoka kwenye nafasi ya Usemaji akiwa amechangamka kwa kuwa kuna wakati wizara nne zilikuwa zinapigwa na anapaswa kutoa majibu kwa haraka.
“Nimeona uzalendo ndani ya waandishi, kuna wakati mtu asiyefahamu inakuwa kama vita anakwambia waandishi wenu hawa, mtu asiyeelewa hii sekta lakini tulipata shida hapa Kariakoo, kuna vitu ambavyo sitasahau nilikaa siku tatu pale hatujaondoka na ni janga la kitaifa.”
“Humu baadhi yenu tulikesha nao na wanauliza tufanye nini ili jamii iweze kutulia. Hakuna uzalendo kama huu kwa sababu mwandishi kalamu au picha yake inaweza kubomoa jamii lakini nimeona uzalendo wa hali ya juu,”alisema.
Aliwaomba waandishi kuendelea kutumia kalamu zao kujenga taifa lenye mshikamano huku akimuahidi Rais Samia kuwa atatumia vipaji vyake kuhakikisha analitumikia taifa ili kuchochea maendeleo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED