Madaktari Bingwa wa Dk. Samia wawasili Shinyanga, kutoa huduma za matibabu bure

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 01:46 PM Jun 17 2024
Mratibu wa Timu ya Madaktari Bingwa Dk.Everine Maziku akizungumzia ujio wa Madakatari Bingwa Mkoa wa Shinyanga.
Picha: Marco Maduhu
Mratibu wa Timu ya Madaktari Bingwa Dk.Everine Maziku akizungumzia ujio wa Madakatari Bingwa Mkoa wa Shinyanga.

KAMBI ya Madaktari Bingwa kupitia Kampeni ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi, imewasili mkoani Shinyanga tayari kwa kutoa huduma kwa wananchi.

Madaktari hao Bingwa wamewasili leo Juni 17,2024 ambapo watatoa huduma za kibingwa kwa wananchi katika halmashauri zote sita za mkoa huo kwa siku tano hadi Juni 22.

Mratibu wa timu hiyo, Dk. Everine Maziku kutoka Idara ya Afya,Uzazi,Mama na Mtoto Wizara ya Afya, amesema madaktari hao wapo 30, na watawafikia wananchi wote ambao watafika kupatiwa huduma hizo za kibingwa.

Amesema tangu madaktari hao waanze kutoa huduma hizo za kibingwa, tayari wameshafika katika mikoa 20 na kutoa huduma za matibabu kwa wananchi zaidi ya Elfu 50, pamoja na kuwajengea uwezo watoa huduma za Afya wapatao 3,500.

1


“Huduma ambazo zitakuwa zikitolewa na madaktari hawa ni magonjwa ya wanawake, watoto, upasuaji,mkojo,ganzi,usingizi, macho, mifupa, mionzi na magonjwa ya ndani,” amesema Dk.Everine.

Muuguzi Mkuu Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, Frola Kajumla, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile, amemshukuru Rais Samia kwa kufikisha timu hiyo katika mkoa huo, na kuwafikia wananchi hadi wa pembezoni kupata huduma za kibingwa na kuimarisha Afya zao.
2

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga, wajitokeze kwa wingi kwenye Kambi za madaktari hao bingwa, ambao wamesambaa kwenye halmashauri zote ili wapate matibabu ya kibingwa.

Nao baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Shinyanga  wamemshukuru Rais Samia, kwa kuendelea kujali wananchi wake kwa kuhakikisha wanaendelea kuwa na Afya Njema, kwamba licha ya kuboresha huduma za Afya nchini, bado ameendelea kuwapelekea na Madaktari Bingwa hadi pembezoni mwa Miji.