DC asisitiza utoaji elimu usalama barabarani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:39 PM Jun 17 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kilindi   Hashim Mgandilwa akizungumza alipokuwa akifungua mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva bodaboda.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Hashim Mgandilwa akizungumza alipokuwa akifungua mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva bodaboda.

MKUU wa Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga Hashimu Mgandilwa amesisitiza wadau mbalimbali likiwemo Shirika la Amend kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva bodaboda wa wilaya hiyo ili kupunguza ajali na kuliwezesha kundi hilo kufanya shughuli zake kwa kufuata sheria.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya usalama barabarani yaliyokuwa yakiendeshwa na Amend kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswis, Mgandilwa amesema anashukuru kutolewa kwa mafunzo hayo katika wilaya yake kwani watumiaji wengi wa vyombo vya moto na hasa pikipiki hawana elimu ya usalama barabarani.

“Sehemu kubwa ya waendesha vyombo vya moto hawana elimu ya usalama barabarani lakini pia kundi ambalo halina elimu hiyo ni kundi la bodaboda. Hivyo ofisi yetu kwa kushirikiana na VETA-Kilindi tuliandaa  mafunzo kwa vijana 100 ambao walipatiwa mafunzo.

“Pamoja na kutolewa mafunzo kwa kundi hilo la vijana 100 bado tumefungua milango kwa watalaam na mashirika mengine kuja kutoa elimu hii na sasa tunashukuru Amend mmeitoa mwito wetu na leo nafungua mafu nzo ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda,” amesema Mgandilwa.

Ameongeza katika mafunzo hayo yanakwenda sambamba na utolewaji wa elimu ya huduma ya kwanza ili itakapotokea ajali angalau kuwepo na uelewa wa huduma ya kwanza kumsaidia aliyepatwa na changamoto.

Azungumza zaidi katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika vituo vinne vya Songe Mjini, Kwa Madoti, Kibirashi na KwediBoma Mgandilwa amesema waendesha pikipiki zaidi ya 180 wameshiriki katika kampeni hiyo ya elimu ya usalama barabara kwa bodaboda.

“Nawashukuru Amend na nawaomba muendelee kutoa elimu hiyo kwa vijana wengine kwani mahitaji ni makubwa na mafunzo yanahitajika kuwa kila siku vijana wengi wanaingia kwenye biashara ya bodaboda.”

Kwa upande wake Mratibu wa Shirika la Amend Ramadhan Nyanza amesema wanamshukuru Mkuu wa Wilaya ya Kilindi kwa kuona umuhimu wa mafunzo hayo ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda na hatua ambazo amekuwa akichukua ikiwemo ya kushirikiana na wadau kama VETA kutoa mafunzo hayo kwa vijana 100 kama sehemu ya kupunguza ajali za barabarani.

 “Amend kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswis nchini tunatarajia kufika maeneo mengi zaidi kutoa mafunzo ya usalama barabarani kupitia kampeni hii.Malengo yetu ni kuwafikia vijana wengi zaidi.”

Wakati huo huo baadhi ya vijana waliopata mafunzo hayo, akiwemo Shaban Juma na Hussein Mhando wamesema wanatoa shukrani kwa Mkuu wa Wilaya pamoja na Amend kwa kuona muhimu wa wao kupatiwa mafunzo hayo.

Wamesema wanaamini yatasaidia kupunguza ajali za barabarani huku wakikiri wengi wanaendesha pikipiki lakini hawana elimu ya usalama barabarani na hivyo baadhi yao kuwa chanzo cha ajali zinazosababisha ulemavu na wakati mwingine vifo.