490,000 wapewa msaada wa kisheria, migogoro yatatuliwa

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 03:56 PM Jul 06 2024
Kazi ya kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi ikiendelea katika viwanja vya sabasaba kwenye banda la Mama Samia Legal Aid Campain
Picha: Elizabeth Zaya
Kazi ya kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi ikiendelea katika viwanja vya sabasaba kwenye banda la Mama Samia Legal Aid Campain

WANANCHI 490,000 kutoka katika mikoa saba, wametatuliwa migogoro yao mbalimbali kupitia Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, iliyopewa jina la Mama Samia Legal Aid Campaign huku migogoro ya ardhi ndio ikiongoza.

Kaimu Mkrugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na Nipashe kwenye banda la Mama Samia Legal Aid Campaign katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaama(DITF) yanayoendelea barabara ya Kilwa wilayani Temeke.

Ester ambaye pia ni Msajili wa Mashirika yanayotoa huduma za msaada wa kisheria, alisema baadhi ya migogoro ambayo imetatuliwa kupitia kampeni hiyo ni ile inayohusu ushauri wa msaada wa kisheria, kuelimishwa kwa suala lolote la kisheria pale wanapohitaji kuwasilisha mahakamani, kuwaunganisha na Mawakili, kuandaliwa nyaraka na huduma nyinginezo zinazohitaji kutatuliwa kisheria.

"Kwa hiyo Wizara iliona umuhimu wa kuleta kampeni hii ya kitaifa ya msaada wa kisheria ambayo imepewa jina mama Samia legal Aid Campain  katika maonesho haya ya sabasaba kutokana na umuhimu wake katika kutatua migogoro ya wananchi na kampeni hii inatolewa bure,"alisema Eater.

"Kwa hiyo tuko hapa kuungana na wadau wengine katika kuhakikisha mwananchi hakosi huduma yoyote ya kisheria akiwa katika viwanja hivi vya sabasaba, kwa hiyo kama kuna mtu ana jambo lake linamtatiza na anataka litatuliwe kisheria atumie fursa hii ya maonesho,tuko mpaka mwisho kuhakikisha tunawafikia wananchi wengi zaidi."

Alisema kesi ambazo wakili anaweza  kumsaidia mwananchi baada ya kufika katika kampeni hiyo ya kitaifa ni pamoja na hati za kufungua mashauri mahakamani iwe ni kufungua kuomba usimamizi wa mirathi, masuala ya madai,matunzo ya watoto, kuasili watoto na masuala mengine ya kisheria ambayo nyaraka zake zinapelekwa mahakamani.

Alisema pia ipo mikataba ambayo mtu anaweza kusaidiwa kuandika pamoja na huduma nyingine ambazo mwananchi wa kawaida hawezi kwenda kuzipata kutokana na kutokuwa na uwezo wa kumlipa wakili.


Ester alisema tangu yalipoanza maonesho ya sabasaba Juni 28 mwaka huu, mwitikio wa wannachi wanaojitokeza kuomba kutatuliwa migogoro yao inayohitaji msaada wa sheria ni mkubwa.


"Wananchi waliojitokeza ni wengi tangu tumefika hapa Juni 28 na  hii inatuonyesha kwamba huduma zetu zimefika mbali sana na wananchi wamepata taarifa,"alisema Ester.

Mama Samia Legal Aid Campain ilianza kutekelezwa mwaka jana Aprili kwa kuanzia mkoani wa Dodoma na mpaka sasa tayari mikoa saba imefikiwa.