WATAALAMU wa ununuzi na ugavi wametakiwa kuzingatia sheria za manunuzi na kutumia mfumo wa manunuzi wa kielektroniki (NeST) ili kuongeza uwazi na ubora katika miradi ya serikali.
Wataalamu hao pia wameonywa kujiepusha na rushwa kwa kuwa vitendo hivyo vitachelewesha ununuzi na kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuiingizia serikali hasara ya mabilioni ya fedha.
Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Musa, alisema hayo jana jijini Arusha, wakati akifunga Kongamano la 15 la Wataalamu wa Bodi ya Ununuzi na Ugavi (PSPTB) lenye kauli mbinu ya mabadiliko ya ununuzi na ugavi kwa usimamizi bora wa rasilimali na kuhudhuriwa na washiriki 1,900.
“Katika siku tatu za kongamano hili mmepata fursa ya kujifunza, kubadilidilishana uzoefu na kuweka mikakati kusadia sekta ya ununuzi na ugavi na kuwa na tija kwa taifa. Hivyo mnapotoka hapa nendeni mkawe chachu ya mabadiliko chanya katika maeneo yenu ya kazi kwa kukata rushwa na kutumia NeST kuongeza ufanisi wa miradi,” alisema Musa.
Alisema kongamano hilo limeazimia kupunguza changamoto zilizopo kwenye fani ya ununuzi na ugavi nchini.
“Ni vema yakapewa nafasi ya kutosha katika maeneo yenu ili kufikia malengo ya serikali yaliyokusudiwa, lakini pia yakawe dira ya kuwaongeza katika majukumu yenu ya kila siku,” alisema.
Alitoa mfano kuwa Mkoa wa Arusha kwa kipindi cha mwaka mmoja umepokea fedha zaidi ya Sh. trilioni 2.7 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Alisema endapo wataalamu hao hawatatimiza wajibu wao, miradi hiyo haiwezi kutekelzwa kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
"Naomba hakikisheni mnatoa huduma bora kwa Watanzania kwa kuzingatia ununuzi wa thamani ya fedha iliyotolewa.
“Ninawaomba mkatoe huduma bora kwa Watanzania kwa kuzingatia ununuzi wa thamani ya pesa iliyotolewa ionekane kwenye miradi hiyo”.
Kwa upande mwingine, aliwataka wataalamu hao kuepuka adhabu zisizo za lazima, huku akiwasisitiza waajiri kutenga fedha za kuwajenga uwezo ili waendelee kutekeleza majukumu yao kitaalamu zaidi.
Makamu Mwenyekiti Bodi Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Benezeth Ruta aliwasisitiza wataalamu hao kuheshimu na kuzingatia sheria za ununuzi na ugavi ili nchi iweze kufikia malengo ya uchumi yanayokusudiwa.
“Kongamano letu lilijielekeza kujadili mabadiliko ya kidijitali kwa maendeleo endelevu ya taifa. Ninawaomba mkazingatia maadili na kutanguliza uzalendo mbele kwa kuwa sekta hii ni injini ya nchi kutekeleza miradi ya maendeleo,” alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED