WAFUGAJI 97 wa jamii ya Kimasai, waliokubali kuhama kwa hiari ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), wametoa angalizo kwa waliobaki kuwa ni hatari kuishi na wanyama wakali katika eneo moja.
Mwitikio uliopo sasa wa wananchi kukubali kuhama Ngorongoro, kupisha shughuli za uhifadhi, umesaidia kupunguza shughuli za kibinadamu hifadhini, kukosa uhuru wa kumiliki vyombo vya moto, kufanya shughuli za kiuchumi na uhuru wa kutembea ndani ya hifadhi baada ya saa 12 jioni.
Kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wafugaji hao, akiwamo Daudi Melubo, Mkazi wa Kijiji cha Kayapus, alisema ameamua kuondoka kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera Kata ya Misima Wilaya ya Handeni mkoani Tanga ili yeye na familia yake kupata uhuru nje ya Ngorongoro.
Melubo na wenzake, sasa wanakuwa kundi la 21 la awamu ya pili lenye kaya 23, watu 97 na mifugo 196 kuhama ndani ya hifadhi hiyo kuelekea Msomera na maeneo mengine waliyochagua wenyewe.
Mbali na Msomera, Saunyi (Kilindi), wananchi wengine wamehamia Wilaya za Monduli (Arusha), Meatu (Simiyu) na Simanjiro (Manyara).
“Nimeamua kuhama kwa hiyari yangu kwenda Msomera kwa sababu huko kuna uhuru wa kujiendeleza, nitajenga nyumba, nitamiliki ardhi, watoto wangu wataenda shule bila hofu ya mnyama mkali na hakuna sheria kama hifadhini,” alisema.
Naishiye Sembeta alisema kuwa: “Sisi wanawake tumekuwa tukitembea umbali mrefu kwenda kutafuta kuni porini huku tukihatarisha maisha yetu, ila sasa tunahamia Msomera na tunaamini maisha yetu yatabadilika na kuwa bora zaidi.”
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi hilo, Meneja wa Mradi, Ofisa Uhifadhi Mkuu wa NCAA, Florah Assey, alisema hadi kufikia Desemba 19, mwaka huu, kaya 1,678 zenye watu 10,073 na mifugo 40,593 zimehama ndani ya hifadhi hiyo kuelekea Msomera na wengine maeneo waliyochagua wenyewe.
Kwa mujibu wa Florah, utaratibu uliopo ni kuhakikisha kuwa zoezi la uandikishaji, tathmini ya maendelezo na uhamishaji vinaenda sambamba ili kila mwananchi atumie muda mfupi kuhama ndani ya hifadhi hiyo na kwenda eneo alilochagua.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED