Rushwa Minjingu funga kazi, Kamishna TRA aambiwa

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 09:48 AM Dec 21 2024
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda.
Picha: Mtandao
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda.

WAFANYABIASHARA mkoani Manyara wamemwomba Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda kuwadhibiti baadhi ya watumishi kwa kuomba rushwa kwenye vizuizi ili kuvusha bidhaa zao.

Ombi hilo walilitoa jana mjini hapa, wakati wakizungumza na Kamishna Mwenda.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Manyara, Musa Msuya, alidai licha ya mazingira mazuri yaliyowekwa na serikali ya awamu ya sita kufanya biashara, kuna tatizo kwenye kizuizi cha Minjingu kwa  wao kuombwa rushwa ili kuruhusiwa kuvusha  bidhaa zao. 

"Tukiagiza mizigo Arusha haivuki Makuyuni, tunalazimishwa kutoa rushwa,  ni lazima uandae Shilingi 200,000 za kuhonga ili kuruhusu mzigo utoke," alidai Msuya. 

Aliendelea kudai kuwa kuna wakati aliagiza bidhaa Arusha, gari lake lilikamatwa na kuzuiwa kwa saa zaidi ya 10 na watumishi hao na kukubali kutoa rushwa ili liachiwe. 

Licha ya vikwazo hivyo, awali alisema malalamiko mengi dhidi ya TRA yanatatuliwa kwa wakati na wanalipa kodi bila kutumika mtutu wa bunduki. 

"Zamani tulikuwa tunakusanya kodi kama vile tuko vitani na watumishi wa TRA, tulikuwa hatuwezi kukaa nao hata kunywa soda," alisema Msuya. 

Mfanyabiashara mwingine, Abeid Baiday, alidai rushwa inayotajwa  Makuyuni na Minjingu ipo kizuizi cha Katesh na kwamba  iliyopo Minjingu ndio funga kazi. 

Baiday, alidai gari linashikiliwa bila kosa mpaka liachiwe mtu anatakiwa atoe rushwa. 

"Mimi pale Minjingu natamani niende na fimbo niwachape viboko maana wamezidi kwa rushwa," alidai.

Akijibu madai ya wafanyabiashara hao,  Mwenda alisisitiza kuwa watumishi wa TRA wanalipwa mishahara na serikali na wapo kuwahudumia wafanyabiashara na siyo kuwaomba rushwa. 

Aliwataka wafanyabiashara wasikubali kutoa rushwa kwa watumishi hao na kuchukua ushahidi kisha kuwaripoti kwa wakuu wao wa kazi ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao. 

Alisema ametoa maelekezo kwa Meneja wa Mamlaka hiyo wa mkoa kushughulikia madai hayo dhidi ya watumishi hao ili hatua zichukuliwe dhidi yao na kuwaondolea kero wafanyabiashara kwenye vizuizi hivyo.

Alisema tuhuma hizo za rushwa ni miongoni mwa vigezo ambavyo meneja wa mkoa wa TRA anapimwa kwenye utendaji ni kuzalisha biashara nyingi na siyo kuua biashara.

Kuhusu wafanyabiashara kukaguliwa hesabu za miaka 10 iliyopita, alisema walikubaliana iwe ndani ya miaka mitatu.

Vilevile Mwenda, aliwataka wafanyabiashara wenye matatizo ya kulipa kodi  kukutana na meneja wa mamlaka hiyo kukubaliana kulipa kwa awamu bila usumbufu.

Kamishna huyo wa TRA, alitembelea Kampuni ya Mati Super Brands Limited na kuipatia tuzo ya heshima baada ya kulipa kodi Sh. bilioni tano kwa miezi mitano.

Alisema wataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kampuni hiyo ili kufikia malengo yake kwa kuwa ni mlipakodi mkubwa wa kitaifa. 

 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, David Mulokozi, aliipongeza TRA kwa kuwapatia ushirikiano na kukua kwa kasi na kusambaza bidhaa zao mpaka nje ya nchi.