WAKATI zikiwa zimesimama kwa muda kucheza mechi za Ligi Kuu wiki hii kutokana na kuwa na majukumu ya mechi za kimataifa, Mabingwa Watetezi Yanga wameonekana kuvuna pointi nyingi ikicheza ugenini, huku Simba ikipachika mabao mengi ikicheza nyumbani.
Kwa mujibu wa takwimu za dawati la michezo la gazeti hili, Yanga pamoja na kushika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na pointi 27, inaongoza kwa kuzoa pointi nyingi ugenini, ikiwa imekusanya pointi 18.
Timu hiyo imekusanya pointi tisa tu ikicheza kwenye uwanja wake wa nyumbani.
Yanga imecheza michezo sita ikiwa ugenini, ikishinda yote, ikifunga mabao manane, na kutoruhusu bao lolote.
Imecheza michezo mitano nyumbani, ikishinda mitatu na kupoteza miwili, ikifunga mabao manane na kuruhusu manne.
Yanga inafuatiwa na Azam FC, ambayo imekusanya pointi 17 ikicheza ugenini, imecheza mechi saba, imeshinda michezo mitano, sare mbili na haijapoteza mechi yoyote.
Katika michezo yake ya nyumbani, Azam, imeshuka dimbani mara sita, ikishinda mara nne, sare moja na kupoteza mmoja mbele ya Simba kwa mabao 2-0, mechi ikichezwa, Uwanja wa New Amaan Zanzibar, Septemba 26, ambapo Wanalambalamba waliutumia kama uwanja wao wa nyumbani.
Simba inashika nafasi ya tatu ikizoa pointi 15 ugenini, Singida Black Stars ni ya nne ikiwa imekusanya pointi 13.
Wakati hayo yakiendelea, timu ya Simba inaongoza kwenye Ligi Kuu kwa kufunga mabao mengi ikicheza uwanja wake wa nyumbani.
Simba imepachika mabao 16, kati ya 22 ambayo imeyafunga mpaka sasa, ikicheza nyumbani ambapo imeshuka dimbani mara sita, ikishinda nne, sare moja na kupoteza mchezo mmoja dhidi ya Yanga.
Timu ya Fountain Gate inafuatia kwa kupachika mabao mengi ikiwa nyumbani, ikifanya hivyo mara 12, kati ya 20 iliyofunga kwenye Ligi Kuu mpaka sasa.
Timu hiyo inafuatiwa na Yanga pamoja na Azam zinashika nafasi ya tatu ambazo zote zimepachika mabao manane kila moja ikicheza viwanja vya nyumbani.
Timu za JKT Tanzania, Dodoma Jiji, Singida Black Stars, na Coastal Union zipo kwenye nafasi ya nne kwa kufunga mabao mengi nyumbani, zikifunga mabao saba mpaka sasa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED