VIONGOZI wa Klabu ya Simba na Coastal Union wamekutana jana mchana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuzungumza kuhusu sakata la usajili la mchezaji Lameck Lawi ili kufikia makubaliano kama walivyoagizwa na Kamati ya Hadhi na Sheria ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Agizo la kikao hicho lilitolewa na kamati hiyo kupitia kikao chake kilichofanywa siku kadhaa nyuma kufuatia mvutano wa usajili wa beki huyo.
Ikumbukwe Simba ilitangaza kumsajili beki huyo na kulipa fedha za usajili kwa Coastal Union lakini uongozi wa klabu hiyo ya Tanga ulikanusha taarifa hiyo na kudai Simba walivunja makubaliano yao ya awali ya usajili wa nyota huyo na kuleta mvutano kabla ya sakata hilo kupelekwa TFF.
Akizungumza na Nipashe jana, Mwenyekiti wa Klabu ya Coastal Union, Steven Mguto, alisema baada ya kikao hicho majibu yatarudishwa katika kamati hiyo ili iweze kutoa maamuzi yake.
"Leo (jana) Simba na Coastal wanakutana mchana huu kuzungumzia suala la Lameck Lawi watakayokubaliana watayapeleka kwenye kamati ili itoe maamuzi yake," alisema Mguto.
Alisema kwa kuwa kikao hicho kinafanyika kwa maagizo ya kamati ya TFF, wao (kamati hiyo) ndio watakaozungumza kutokana na kile klabu hizo watakachokuwa wamekubaliana.
Katika hatua nyingine, Mguto alisema timu yao kwa sasa inaendelea na kambi ya mazoezi Visiwani Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Ngao ya Jamii utakaochezwa Agosti 8 mwaka huu dhidi ya Azam FC.
Alisema malengo yao ni kufanya vizuri kwenye mchezo huo ambao ni maalum kwa ajili ya ufunguzi wa msimu wa Ligi Kuu itakayoanza Agosti 16.
"Malengo yetu ni kufanya vizuri katika michezo yetu yote tukianzia na ile ya tarehe nane kwani kikosi tulichonacho tuna imani tutafanya vema," alisema Mwenyekiti huyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED