Mawakala wa Vinícius wataka mshahara mkubwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 01:06 PM Feb 16 2025
Vinícius Júnior
Picha: Mtandao
Vinícius Júnior

MAWAKALA wa Vinícius Júnior wameiarifu Real Madrid kuhusu mahitaji ya mshahara wa mteja wao kama ataendelea na klabu hiyo baada ya mwaka 2027, kwa mujibu wa chanzo cha ESPN.

Wawakilishi wa mchezaji huyo wana matumaini ya kukutana na viongozi wa Madrid katika siku zijazo ili kuendelea na majadiliano.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Vinícius anakaribia kurefusha mkataba wake huko Madrid kuliko kuhamia Saudi Arabia, kama inavyoripotiwa kwenye vyombo vya habari vya Hispania.

Ligi ya Saudi Arabia inataka kumfanya fowadi huyo wa Brazil kuwa mchezaji anayelipwa fedha nyingi zaidi duniani, lakini vyanzo viliongeza kuwa tangu Desemba hakujakuwa na taarifa zozote kuhusu uhamisho huo.

Ingawa chanzo hakikufichua mahitaji maalum ya kifedha ya Vinícius kubaki Madrid, lakini imaaminiwa kwamba mchezaji huyo anataka mshahara mkubwa zaidi ya Kylian Mbappé na Jude Bellingham.

Mkataba wa sasa wa Vinícius unamalizika mwaka 2027 na kama ESPN ilivyoripoti hapo awali, mshahara wa mchezaji huyo unakaribia euro milioni 10 kwa msimu pamoja na nyongeza.

ESPN iliripoti wiki iliyopita kwamba Madrid ilikuwa imekutana na wasaidizi wa Vinícius kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya kuongeza mkataba.

Chanzo hicho kinaongeza kuwa Vinícius hana haraka ya kufanya hivyo licha ya kuzungumza hadharani kuhusu nia yake ya kuendelea kubakia Madrid kwa muda mrefu.

***