KLABU ya JKT Tanzania imekuwa timu pekee iliyopata ushindi mkubwa zaidi katika mechi za raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), maarufu Kombe la FA katika mechi sita zilizopigwa juzi kwenye viwanja mbalimbali ikiikandamiza Igunga FC mabao 5-1.
Baada ya ushindi huo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Masau Bwire alisema hilo ni onyo kwa timu zingine zinazoshiriki michuano hiyo.
Masau amesema msimu huu wamedhamiria kufanya vyema kweli Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho hivyo kuzitahadharisha timu itakazopangwa nazo kwenye Kombe la FA kutarajia kipigo kama hicho.
"Ni kipigo tulichotarajia kuwapiga, kwa sasa hatuna shaka, timu yoyote itakayopata bahati mbaya ya kukutana na sisi itarajie kuwakuta kilichowakuta Igunga FC," alisema Masau.
JKT Tanzania ilikuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani, Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam, ikipata ushindi huo na kufanikiwa kutinga hatua ya 16 bora.
Nahodha wa kikosi hicho, John Bocco aliwaongoza vyema wenzake, akiwa mmoja wa waliofunga mabao hayo, dakika ya 14, likiwa ni bao la pili kwenye mchezo huo, likitanguliwa na bao la Wilson Nangu dakika ya 12, Mohamed Bakari, akifunga mabao mawili, dakika ya 16 na 30, huku Dany Lyanga akipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la wageni wao kutoka Tabora.
Timu zingine zilizopata ushindi na kutinga hatua hiyo, ni Cosmopolitan iliyoichapa Nyota Academy mabao 2-0, Stand United nayo ikapata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Don Bosco, Polisi Tanzania ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bukombe Combine huku, Namungo nayo ikipata ushindi nyumbani wa mabao 2-0 dhidi ya Tanesco FC.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED