NIMEBAHATIKA kuhudhuria mkutano wa wadau wa habari kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.
Mkutano huo ulioandaliwa na Wizara ya Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, ulipokea mada mbalimbali kuhusu wajibu wa vyombo vya habari kwenye uchaguzi. Moja ya mada hizo ni wajibu wa vyombo vya utangazaji kwenye uchaguzi, iliyowasilishwa na Mhandisi Andrew Kisaka kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Vyombo vya utangazaji vinatakiwa kutoa elimu kwa mpigakura, kufahamisha umma mwenendo wa kampeni za vyama vya siasa, kuripoti hali halisi siku ya kupigakura na kutangaza matokeo.
Malengo ya kanuni hizi ni kuweka mizania ya matangazo ya vyama vya siasa wakati wa uchaguzi, kuhamasisha weledi na maadili ya utangazaji, kuhamasisha uwazi, mizani na kutobagua kundi lolote katika jamii na kuhakikisha kuwa vyombo vya utangazaji haviegemei upande wowote.
Kanuni hizi zinaelekeza katika kuripoti habari za uchaguzi, utangazaji wa habari zote wakati wa uchaguzi wa vyama vya siasa unaripotiwa na kuwasilishwa bila upendeleo na kwa uadilifu bila kuonyesha mtazamo binafsi wa mtangazaji. Vyombo vya Utangazaji vinapaswa kutoa haki sawa kwa vyama vyote bila upendeleo na kwa uwiano usawa, kwa usahihi na kuripoti matukio ya kisiasa kwa uadilifu na weledi bila upendeleo.
Mchakato mzima wa uchaguzi uazimie kusisitiza umuhimu wa uchaguzi na kuhamasisha ushiriki wa wananchi wote katika mchakato wa uchaguzi; na katika kipindi cha uchaguzi, habari zinalenga masuala yanayowanufaisha wananchi hususani sera za vyama na mikakati waliojiwekea kama watapewa nafasi ya kuongoza.
Uwasilishaji wa vipindi vya uchaguzi unapaswa kuwa unaendana na sera, sheria na kanuni zinazoongoza utendaji kazi wa vyombo vya habari vya kielektroniki. Usiwe na upotoshaji wa taarifa binafsi au usingiziaji wa mgombea yeyote au mtu mwingine, au maoni yoyote yasiyofaa juu ya sifa njema za mtu yeyote; hauhusishi maoni ya kisiasa yaliyojengeka katika ubaguzi wa kimbari, rangi, ulemavu, dini, imani, jinsia au eneo analotoka mtu.
Aidha, vipindi havitahusisha lugha yoyote ya kukashfu, uvunjifu wa sheria au lugha ya kukufuru au lugha yoyote inayoweza kusababisha vurugu au uchochezi wa maasi; vipindi havitahusisha utoaji wa maoni yoyote yanayoweza kuumiza hisia za mtu yeyote kutokana na jinsia yake, jinsi, mbari, rangi, tabaka, imani au eneo analotoka, matangazo ya chama cha siasa yatakuwa ni yale tu ambayo vyama vinataka kunadi sera zake, programu na malengo yake.
Kanuni hizi zimetoa wajibu wa kutangaza bure habari na vipindi vya uchaguzi kwa vyombo vya utangazaji vya umma pekee, yaani public broadcasting stations, kwa maana hiyo, hii maana yake ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) pekee.
Nikiwa mwandaaji wa maudhui, kupitia kampuni yangu ya PPR, nimeandaa maudhui ya elimu kwa umma kupitia vipindi sita vya televisheni na sita vya redio na kuviwasilisha TBC na kuwanakili TCRA.
Ili vyombo vya habari vyote viwatendee haki Watanzania wakati wa uchaguzi, hatua ya kwanza ni kuwezeshwa. Japo jukumu la kutangaza bure habari ni jukumu la vyombo vyote vya habari, jukumu la kutangaza vipindi vya bure limeachwa kwa vyombo vya habari vya umma pekee na hakuna kipengele chochote kinachozungumzia uwezeshaji wa vyombo vya habari kutumiza wajibu.
Nilizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk. Ayub Rioba, na baada tu ya kumweleza kuhusu vipindi hivyo, alikubali TBC kuvipokea na kunielekeza kuvikabidhi kwa mkuu wa vipindi ili kuangalia maudhui na wakijiridhisha vitarushwa hewani.
Kwanza nitoe pongezi kwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC kwa kunipokea na kunikubalia leta vipindi tuviangalie. Hii ni hatua kubwa ya kustahili pongeza hata kama mwisho wa siku, vipindi havitarushwa. Ile nia njema tu ya ruhusa ya TBC kupokea vipindi ni jambo jema.
Pia nitoe pongezi kwa Mkuu wa Vipindi TBC, Happiness Ngasala, kunipokea na kuvipokea vipindi vyangu lakini pia ili TBC itimize majukumu yake kikamilifu, hata TBC inatakiwa kuwezeshwa, ili kutoa hiyo muda wa kurusha matangazo au vipindi bure kwa elimu kwa umma na kwa vyama vya siasa.
Uwezeshaji huu usiishie kwa TBC tu. Kanuni inaelekeza vituo binafsi vya utangazaji, kupanga bei rafiki kwa vyama vyote vyenye uwezo wa kulipia, virushe vipindi vyao.
Kwa vile hali za uchumi wa vyama hazifanani, kuna vyama vina nguvu za kiuchumi kumudu kulipia vipindi vyao na kuna vyama, haswa ambavyo havipati ruzuku, hali zao ni taabani, haviwezi kumudu hata gharama za kuandaa maudhui, licha ya gharama za kuvilipia, hivyo matangazo ya vipindi yatakuwa ya vyama tajiri na vyenye uwezo pekee.
Watanzania wana haki ya kusikia sera za vyama vyote bila ubaguzi. Serikali , mamlaka ya mawasiliano na wadau wabuni njia za kuziwezesha vyombo vyote vya umma na binafsi wakati wa uchaguzi, Kutenda haki sawa kwa vyama vyote na kuwapa Watanzania haki ya kusikia sera za vyama vyote bure bila vyama kulazimika kulipia bila TBC kubebeshwa mzigo wote wa kurusha vipindi vya bure bila kuwezeshwa.
Nawatakia Watanzania, uchaguzi mwema wa serikali za mitaa.
Mungu Ibariki Tanzania.
Paskali.
+255 754 270403
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED