MAPENZI ni ridhaa ya mtu mwenyewe kutamani au kumpenda mwingine. Hakuna yeyote anayelazimishwa au kushikiwa fimbo kupenda. Mapenzi huwa yanazuka tu na wala hayajulikani yametokea wapi.
Mtu anaweza kumpenda yeyote yule bila ya kuwa na kitu chochote kile ambacho kimemvutia. Yeyote anayempenda mtu kwa sababu ya kitu, basi penzi lina matatizo hilo. Siku kitu alichompendeza kitatoweka, mapenzi yanakufa kifo cha asili.
Mapenzi ni hisia tu. Mwanamume anaweza kuwaona wanawake hata 100, lakini akatokea mmoja akavutiwa naye na anayempenda atashindwa kuainisha ni nini haswa alichompendea. Anaweza kubabaisha tu lakini ukweli kitu halisi kinakuwa kwenye ubongo wake.
Mwanamke naye anaweza kutongozwa na wanaume hata 100, akawakataa wote. Akatokea mmoja tu wa 101, akamkubali kwa sababu ambazo anaweza kuziainisha, lakini ukizifutilia unaweza kukuta sifa hizo hata aliowakataa wanazo.
Amemkubali kwa sababu ambazo hata yeye mwenyewe hazifahamu vizuri. Ni hisia tu. Kwa maana hiyo mapenzi ya mtu yapo kwa mtu mwenyewe. Ziko tabia za baadhi ya watu kujifanya walimu wa mapenzi ya watu. Si wanawake si wanaume.
"Kwa nini unampenda yule? Ana nini yule ambacho atakupa wewe? Masikini yule, hana kitu yule. Kwanza ana wanawake wengi, mimi mwenyewe ameshawahi kunitongoza nikamtataa."
Ni baadhi ya maneno ambayo hutoka kwa baadhi ya wanawake ambao hao kazi yao kuingilia hisia na mapenzi za wenzao.
"Yaani ukimkubali nitakuona wewe hamna kitu kabisa shoga yangu, mkubali fulani, yule ana pesa, anakupenda na anakujali." Atampigia debe mwanaume mwingine ambaye labda humpa pesa kwa ajili ya kulaisha mambo.
Asiye na msimamo anaweza kumkataa mwanamume anayempenda kwa sababu za kuambiwa na kungukia kwa aliyelazimishwa kwa sababu ya matakwa au faida ya mtu mwingine.
Wanaume nao ni hivyo hivyo, baadhi yao wanatabia ya kwenda kwa wanawake na kuwalaumu kwa kuwapenda watu wengine.
"Yule atakwambia nini? Hana pesa, ana matatizo kibao, wewe tupende watu kama sisi."
Hawa ni baadhi ya wanaume kwenye tabia hiyo. Kama mwanamke huna msimamo unaweza ukamuacha wako anayekupenda kwa dhati ukaangukia kwake, ambaye hapendi ila anatamani tu.
Wako pia wafitini ambao wanawagombanisha hata watu walio kwenye ndoa. Ndoa nyingi zimevunjika kwa sababu ya watu wa aina hiyo na kuwaacha watoto wanateseka, hawasomi, wanahangaika na wengi wamekuwa ombaomba kisa maneno ya uongo ya kuambiwa.
Ndiyo maana wanandoa na wapenzi siku zote wanaambiwa wasisikilize maneno ya pembeni, ni mabaya sasa. Waamuzi wa penzi lenu ni wao wenyewe. Walipopendana walikuwa wawili tu, iweje leo mtu wa tatu awe mwamuzi wa penzi? Kataa.
Kupendana au kuachana iwe kwa sababu ya sababu zenu wenyewe binafsi na si ushauri au maneno ya watu. Wanamuziki wa dansi wamekuwa wakishauri kwa miaka mingi kuhusu hilo.
Leo tunauangalia wimbo uitwao 'Wajifanya Wajua' uliopigwa na bendi ndogo tu ya Tanga, Amboni Jazz. Pamoja na udogo wake ilifyatua wimbo huo ulioondokea kuwa maarufu, huku mashabiki wakibatiza jina la 'Kidomidomi.' Neno hilo limetumiwa kwenye wimbo huo likiwa na maana ya kidomodomo, likaleta ladha kubwa kwenye wimbo huo.
Katika wimbo huo, mtunzi anamjia juu dada mmoja mmoja mwenye tabia ya kidomodomo na kufitinisha mapenzi ya watu. Wakamwambia maneno haya kwenye wimbo waliouita, 'Kidomidomi.'
Ni kisa cha kweli ambapo mmoja wa wanamuziki hao walimpenda dada mmoja, lakini baada ya watu kuona mapenzi yameanza wakaanza fitina kama kawaida kiasi cha kuyateteresha.
Ilibidi jamaa amfuate mwanamke mmoja anayedaiwa kuwa ndiye kizabizabina na kumpasulia waziwazi aache tabi ya ya ufitini kwani siyo nzuri na anaweza kuadhirika siku moja.
"Wewe wajifanya wajua we dada. Unakuwa mwalimu wa wapenzi wa watu. Mimi nakukanywa, usiwe kidomidomi, utakuja adhirika ulimwenguni humu.
Usipende kashifu watu kwa wapenzi wao, utakuja adhirika dada mitaani, huko si kujenga dada ni kubomoa, mimi sikushauri kitu we dada endelea."
Ni wimbo uliokuwa na maneno mafupi, lakini yenye uzito mkubwa kwa watu wenye tabia kama hiyo.
Tuma meseji 0716 350534
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED