SERIKALI kupitia mamlaka za serikali za mitaa, kwa maana ya halmashauri, imekuwa ikitenga asilimia 10 ya mapato ya ndani, kwa ajili ya kutoa mikopo kwa makundi maalumu ya wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Mikopo hiyo hutolewa kwa makundi hayo kupitia vikundi vilivyoundwa, kwa ajili ya kuwawezesha kufanya uwekezaji katika miradi midogo midogo, ili kujikwamua kiuchumi. Wanufaika wa mikopo hiyo hawatozwi riba bali wanatakiwa kuirejesha kwa muda uliowekwa, ili kuwe na mzunguko na wengine wanufaike.
Aidha, katika maeneo ambayo wawekezaji wanafanya shughuli zao, hutakiwa kurudisha kwa jamii sehemu ya faida wanayopata. Kama ni wachimbaji wa madini, mafuta, kampuni za biashara mbalimbali na viwanda vya kuchakata mazao, wanapaswa kurejesha kiasi cha fedha kinachotokana na faida, kwa jamii inayozunguka uwekezaji huo.
Fedha hizo si lazima ziwe taslimu, bali zinaweza kuonekana kupitia miradi ambayo inasaidia kutatua kero za wananchi walioko katika maeneo husika. Kwa mfano, wawekezajui hao wanaweza kujenga vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, kutoa madawati, kujenga nyumba za walimu na kuchimba visima vya maji.
Pamoja na kuwapo kwa sera hiyo, baadhi ya kampuni zimekuwa hazitekelezi. Kwa hiyo kama serikali inavyofanya kwa kutoa mikopo, kampuni na taasisi kama vile benki, kupitia sera zao za kurejesha kwa jamii (Corporate Social Responsibility- CSR) zitekeleze na zisione ni hisani au huruma bali ni wajibu.
Mikopo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu, imepachikwa jina la ‘Mikopo ya Mama Samia’ na ina lengo la kuwajengea uwezo kwa kuwapatia mikopo ya mitaji. Sera za CSR za kampuni na taasisi kurejesha kwa jamii si hisani, inapaswa itungiwe mwongozo, ili isiendelee kuwa hisani wala huruma bali ni wajibu.
Hivi karibnuni kwenye maonesho ya rasilimali za madini mkoani Geita, Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), ulichangia Sh. milioni 200 kufanikisha maonesho hayo. Ukiangalia fedha hizo zimefanyia nini, unaweza usiamini.
Sehemu kubwa zimetumika kwa posho, kugharimia vyakula, vinywaji na vitafunwa. Kwa maneno mengine, zimeishia ‘Tumbo Street’. Hebu jiulize, fedha hizo kama zinetumika kununua madawati au vitanda hospitalini, wapi ingekuwa na faida zaidi?
Juzi nilihudhuria tukio la utoaji tuzo kwa washindi wa shindano la VIA Creative International Tanzania. Si tu kwamba nimeguswa na kilichofanyika, bali ningetamani kama kampuni zote zinazofanya biashara Tanzania, zitarudisha kwa jamii kitu cha kuonekana na cha kudumu ambacho kitaacha alama.
Katika tuzo hizo, kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania kupitia sera ya CSR, ilifanya kitu kilichoacha alama. Jambo ililofanya ni kwenda kwa jamii na kuuliza changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi.
Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, maarufu kama JPM (Mungu amrehemu), aliwahi kufuta hafla ya mchapalo wa Bunge jipya na kuelekeza fedha zinunue vitanda hospitalini. Akafuta gwaride la Uhuru, fedha zikakarabati barabara ya Morocco – Mwenge.
TotalEnergy Tanzania, imeandaa shindano na shule iliyoshinda, Ubungo Makuburi, itapatiwa si tu zawadi, bali changamoto kuu ya shule yao itajibiwa kwa kujengewa ukuta kuizunguka shule hiyo.
Shindano hilo la kimataifa la ‘VIA CREATIVE’ linanalenga wanafunzi wa shule za msingi wa miaka minne hadi 19, kwa lengo la kuwapatia elimu ya usalama barabarani kwa njia ya sanaa ya michoro, muziki, maigizo na mashairi kisha kuwapa fursa kuelezea uelewa wao na mapendekezo yao ya usalama barabarani, kwa njia ya michoro na maigizo.
VIA Creative ni mradi ulioanza mwaka 2022 ambao tangu mwaka huo, zaidi ya wanafunzi 22,000 wamefikiwa na kujenga klabu za mabolozi wa usalama barabarani kwenye shule 100 Dar es Salaam na Bagamoyo. Mwaka huu mradi huu umewafikia wanafunzi 6,000 kutoka shule za msingi za Makuburi, Ubungo NHC, Buza, Jangwani, Ugindoni na Uzuri mkoani Dar es Salaam na kuendeleza uundaji wa klabu za mabalozi wa usalama barabarani.
Hafla ya kukabidhi tuzo kwa wanafunzi walioshinda kwenye msimu huu wa tatu, ilifanyika kwenye ofisi za kampuni hiyo. Shule ya msingi Makuburi iliibuka mshindi wa kitaifa na mwakilishi wa Tanzania, kwenye ngazi ya kimataifa Novemba, mwaka huu. Shule hiyo pia itazawadiwa kwa kutimiziwa mapendekezo ambayo wanafunzi waliyaomba, kwa ajili ya kuboresha usalama wao barabarani kupitia programu ya VIA Creative.
Mgeni rasmi, Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Kikosi cha usalama Barabarani Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Mrakibu Msaidizi (ASP), Rose Maira, alipongeza TotalErnegies, TotalEnergies Foundation na Nafasi Art Space kwa juhudi na mafanikio yao katika kutoa elimu ya usalama barabarani. Alisema juhudi hizo zinapaswa kupongezwa na kuigwa na kampuni zingine, ili kuchochea usalama wa watoto waendapo na watokapo shuleni.
Pia alionyesha furaha baada ya kujua kwamba mradi huo pia una lengo la kutimiza mapendekezo ya kuboresha hali ya usalama kwa wanafunzi wa shule iliyoshinda, kama ilivyooneshwa kuona kwenye filamu ya wanafunzi hao.
Ni wakati sasa wa kuamka na kutoka usingizini kwa serikali kuweka mwongozo na ufuatiliaji kuhusu taasisi kutekeleza sera zao za CSR. Iwekwe bayana kwamba CSR si fadhila, huruma wala hisani bali ni wajibu wa kampuni na taasisi kutoa sehemu ya faida zinazopata na kurejesha kwa jamii.
Mungu Ibariki Tanzania
Paskali
Mob. +255 754 270403
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED