KATIKA sehemu ya kwanza ya ripoti hii jana, kulikuwa na ufafanuzi wa kina juu ya uhaba wa walimu nchini, nchi ikiwa na walimu 68 tu wenye sifa wanaofundisha somo Uraia kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule za sekondari Tanzania Bara.
Katika toleo la leo, linaangazia uamuzi wa serikali kufuta somo hilo katika shule za msingi na sekondari nchini, wataalamu wakikosoa uamuzi. Sasa endelea...
Wizara ya Elimu, Sayanzi na Teknolojia kupitia maboresho ya mwaka jana ya mtaala na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, imefuta somo la Uraia na kuleta somo jipya linaloitwa Historia ya Tanzania na Maadili.
Wadau wa elimu wametilia shaka uamuzi huo wa serikali wa kulifuta somo la Uraia na badala yake kuleta somo jipya ilhali hakuna walimu wa kutosha waliosomea kufundisha somo hilo katika shule za msingi na sekondari.
Vilevile, wadau hao wanadai kufuta somo la Uraia na kuanzisha somo jipya la Historia ya Tanzania na Maadili kutarudisha nyuma juhudi za kuinua uwajibikaji na uzalendo kwa nchi yao.
Gratian Mukoba, Rais wa zamani wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), anasema haoni somo hilo jipya likijumuisha elimu ya uraia, bali matukio ya kihistoria yaliyorekodiwa tangu utawala wa kikoloni hadi hivi sasa.
"Sioni kama somo hili jipya la Historia ya Tanzania na Maadili linabeba elimu sahihi ya uraia inayopaswa kufundishwa kwa wanafunzi katika ngazi zote.
"Somo Uraia ni muhimu zaidi katika kuunda jamii inayowajibika na kuleta mbadala wake usiozingatia jambo hilo si sahihi," anasema Mukoba, mwalimu mstaafu.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo, Uraia ni somo linalofundisha wajibu wa wananchi kwa taifa lao na haki za msingi wanazopaswa kudai kutoka kwa serikali yao.
Anasema masuala ya kijamii kama vile athari ya rushwa katika uchumi wa nchi, demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu ambayo watoto lazima wafundishwe kuanzia ngazi ya chini ya elimu yao hayabainishwi vizuri katika muundo wa somo jipya la Historia ya Tanzania na Maadili.
"Huwezi kujenga taifa la watu waliostaarabika na kuwajibika kwa kufundisha tu matukio ya zamani ambayo mengi hayana umuhimu katika mtindo wa maisha wa leo," Mukoba anasema.
Mwalimu huyo aliyekuwa anafundisha masomo Uraia, Historia na Kiingereza katika shule za sekondari kuanzia mwaka 1981 hadi mwaka 2017 alipostaafu, anasema Uraia ni moja ya masomo ya siku nyingi yaliyoanza kufundishwa tangu utawala wa wakoloni.
Hata hivyo, mwalimu huyo anaporejea historia ya elimu nchini, anasema somo hilo lilibadilishwa na somo la Siasa mwaka 1965, yaani mwaka mmoja baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kwa mujibu wa Mukoba, baada ya Tanzania kupitisha muswada wa marekebisho ya Katiba ya nchi ya mwaka 1984 na mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, somo Uraia lilirejeshwa kwenye mtaala wa elimu, likifundishwa tena katika shule za msingi na sekondari kuanzia mwaka 1994.
Willbrod Kimaro, mbobevu katika kufundisha somo Uraia, hivi sasa mwalimu wa Shule ya Sekondari Kigamboni, Dar es Salaam, anasema mtaala mpya na sera ya elimu vinaelekeza wanafunzi wa kidato cha kwanza kusoma somo jipya la Historia ya Tanzania na Maadili badala ya Uraia.
"Somo jipya limejikita katika maandalizi ya wananchi wazalendo na waadilifu. Nina matumaini kuwa kutakuwa na kozi za awali za walimu kabla ya kuanza kulifundisha," anasema Kimaro.
Mshauri wa Mambo ya Kitaalamu wa HakiElimu, Dk. Wilberforce Meena, anasema somo jipya la Historia ya Tanzania na Maadili linatilia mkazo zaidi masuala ya maadili kuliko elimu ya uraia.
"Kwa mfano, muhtasari wa somo jipya unaonesha wanafunzi watalazimika kujifunza kuhusu maadili kabla na wakati wa utawala wa kikoloni (1890-1960), baada ya ukoloni (1961-1966), maadili wakati wa Azimio la Arusha 1967-1985 na maadili wakati wa uliberali (1986 hadi hivi sasa," Dk. Meena anasema.
Mshauri huyo anakosoa somo hilo jipya haliambatani na masuala muhimu ambayo yanastahili kufundishwa katika somo Uraia kama vile demokrasia, utawala bora, haki za kijamii, wajibu na haki.
"Uzoefu unaonesha kuwa wizara ya elimu imekuwa na haraka sana katika kuanzisha mawazo mapya, lakini inazembea katika kuweka mazingira wezeshi katika utekelezaji wa mawazo hayo," Dk. Meena anasema.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo bila kutaja kiasi halisi cha fedha, anasema wizara hiyo katika bajeti ya 2023/24, imetenga fedha kwa ajili ya kuchapisha vitabu vya kiada na kutoa mafunzo kwa walimu wa sasa wa somo Uraia ya jinsi ya kufundisha wanafunzi somo jipya - Historia ya Tanzania na Maadili.
"Hakuna haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu mabadiliko haya. Wizara na vyombo vyake vya udhibiti vimeandaliwa vyema. Mchakato wa uandishi na uchapishaji vitabu vya Historia ya Tanzania na Maadili umefanyika kwa umakini mkubwa," anasema Prof. Nombo.
Katibu Mkuu huyo anasisitiza mtaala mpya wa elimu unatekelezwa kwa awamu; ya kwanza itahusisha darasa la awali, la kwanza, la tatu, kidato cha kwanza na kidato cha tano.
Hata hivyo, hadi sasa, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia haijatoa taarifa juu ya idadi rasmi ya walimu waliopatiwa mafunzo ya kufundisha somo jipya la Historia ya Tanzania na Maadili katika shule za msingi na sekondari.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk. Aneth Komba anasema ofisi yake iko tayari kuchapisha vitabu vya kiada vya kufundishia somo hilo.
"Kuhusu uchapishaji na usambazaji vitabu vya kiada, taasisi inahimiza sana matumizi ya nakala laini. Katika kufanikisha mpango huu, taasisi inashirikisha kampuni tatu za simu ili kuwezesha upatikanaji nyenzo za kujifunzia mtandaoni. Bado tunaendelea na mazungumzo nao na tunatarajia kupata hitimisho zuri," anasema Dk. Komba.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED