TAARIFA za habari kwenye televisheni, redio, mitandao ya kijamii zinaarifu kutekwa kwa mtoto wa miaka sita, Macaire, mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule moja Mbezi Dar es Salaam.
(0716 350534)
Mashuhuda wanasema alinyakuliwa na mwanaume mmoja aliyeshiba, kujaa misuli na kukimbilia kwenye gari lililokuwa pembeni mwa barabara ya Bagamoyo, Dar es salaam, ambalo mlango wake ulikuwa wazi.
Wazazi wa mtoto wanapigiwa simu na watekaji wakitaka kiasi cha Sh. Milioni 15 ili wamuachie. Jeshi la Polisi linaingia kazini kumsaka au kuwasaka watekaji. Walichogundua ni kisa cha kushangaza, kusisimua ambacho utakipata utakaposoma kila aina ya nakala ya gazeti hili, ili kuupata mkasa mzima wa tukio.
*************
Dora yeye aligaragara kwenye sakafu ya ofisini, ilibidi waitwe askari watatu wa kile waje kumwinua na kumpeleka ofisi nyingine kwa ajili ya kumbembeleza na kumliwaza.
"Mama mwanangu watamuua leo." Alilia na kuomboleza baada ya kusikia maneno kutoka kwa mzazi mwenzake.
"Unasikia Macky. Sisi tuna uzoefu katika kazi hii kwa miaka mingi. Tayari lengo la hawa watu siyo kuua, siyo viungo vya binadamu. Hawa wanachohitaji ni pesa. Yaani kuwepo hai kwa mtoto kwao wana matumaini makubwa ya pesa. Kifo cha mtoto wako ina maana biashara yote ya kupata pesa kwao itakuwa imekwisha. Hawawezi asilani kwa sababu bado wana nafasi ya kupata pesa kwani mtoto yupo mikononi mwao." Maneno hayo yalimfariji Macky. Aliona kuwa ni kweli kabisa watekaji bado watakuwa wanahitaji pesa kutoka kwake, hivyo hawatumdhuru mtoto kwa sababu wakifanya hivyo, hawatoipata tena.
"Sasa kwa nini wanajua? Kwa nini wanapata habari? Kwa nini kila tunachofanya wanajua? Yaani wale jamaa inaonekana kama hata kama tukifanya kikao hapa wanajua." Akaongea Macky kwa sauti ya msisitizo iliyowashtua maaskari wengine, wakatazamana.
Wakanong'ona, na kwa kauli moja wakaamua kuwaruhusu wazazi hao warejee majumbani kwao na wao wakafanya kikao cha dharura.
Kikao hicho kilikuwa cha askari watatu walioteuliwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Kinondoni kushushulikia mkasa huo.
"Ina maana sisi wenyewe hapa watatu tunageukana au vipi? Afande Chacha akawauliza wenzake. Kila mmoja akakataa na kusema anafanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi.
"Unajua wale ni wazazi, wana uchungu na mtoto wao. Hii ni wiki ya tatu sasa yupo kwenye mikono ya watu ambao hawajulikani. Sisi polisi tuna dhima ya kulinda raia na mali zao. Inakuwaje mpaka sasa huyu mtoto hajarudi kwa wazazi wake? Inawezekana vipi wahalifu wawe na akili kuliko sisi? Inawezekana vipi wawe wanajua maongezi yetu na kila tunachofanya kiasi cha kuweza kujiponya na mkono wa sheria? Inakuje kila mtego unaotega wanaung'amua tena kwa urahisi zaidi kuliko tunavyodhani?" Afande Chacha alizidi kuwamiminia maswali wengine, afande Tom na Pius. Wote walikataa katakata kuwa ni wasaliti. Haikumuingia akilini Chacha.
"Sasa ni nani? Kwanza kabisa tulidhani maongezi yetu yanasikika kwenye simu tunazopiga, tukaambizana wote pamoja na wazazi wa mtoto kuwa wakitaka kuongelea suala hili wasitumie simu. Sisi wenyewe tukapeana maneno ya mafumbo ambayo tulikuwa tunawasiliana tunapotumia mawasiliano wa simu. Tukamuacha mwalimu Kisanga kuwa tusimpe taarifa yoyote baada ya kushuku kuwa anaweza kuwa ndiye mvijisha taarifa kwa bahati mbaya kwani huenda watekaji wanamfahamu na ni watu wake wa karibu kutokana na mazingira ya mtoto alipotekwa. Pamoja na hayo bado wameendelea kujua.
Basi mmoja wetu kati ya sisi watatu anaweza kuwa anahusika kwa njia moja ama nyingine. Ama ndiye mhusika, au anashirikiana na watekaji na kutoa taarifa ya kila tunachokiandaa, kukisema na kukifanya." Afande Chacha alizidi kuwachana wenzake, huku mwenyewe akijua kuwa hahusiki na lolote. Kitendo cha watekaji kujua kila wanachofanya kilimkasirisha sana na kumshushia heshima yake mbele ya wakubwa zake kikazi, wadogo na jamii kwa ujumla. Akafunga kikao hicho. Lakini hakuwa na raha wala amani.
*****************
Kesho yake asubuhi aliamkia kwa bosi wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum kwa ajili ya suala hilo. Akamuelezea kila kitu bila kuacha chochote hata chembe. Alichoomba afande Chacha ni kubadilishiwa askari wenzake. Kwa jinsi alivyoona kamanda ni kwamba akifanya hivyo ataonekana kama imani na wale wawili badala yake anayo kwa mmoja tu ambaye ni Chacha. Aliona haitokuwa vyema kwani hana uhakika kati ya wote ni nane anavujisha siri. Alichofanya alimwambia amletee faili hilo na yeye ndiyo sasa atajua nini afanye.
Baada ya Chacha kutelekeza amri hiyo, alimtaka aendelee na shughuli zingine kwani faili hilo atamkabidhi mtu mwingine.
Aliwaza na kuwazua ampe mtu wingine kwenye ofisi yake, lakini aliona ni kama atakuwa amewafanya wengine pale hawajui kazi, lakini pia hata yeye hakujua ni nani anavujisha siri, inawezekana siyo hao ila ni mmoja wa watu waliomo kwenye ofisi yake. Kupeleka kwa mtu wa kanda nyingine ya Dar es Salaam aliona haiwezekani. Mwishoni wazo likamjia la kumpigia simu bosi mwenzake wa Idara ya Usalama ambaye hufanya naye kazi kwa karibu.
Alimkumbushia sakata la mtoto kutekwa na kwamba kumetokea utata kwenye ofisi yake, hivyo anachotaka asaidiwe kupewa mtu mmoja ambaye anatafanya kazi ya kupeleleza vitu viwili.
Kwanza alipo mtoto alitetekwa na kukamatwa na wahusika wote. Pili kutegua kitendawili cha nani alikuwa anavujisha siri katika majaribio mawili ya kwanza ya kukamatwa kwao.
"Afande, nitakupa kijana mmoja hivi, kwa hilo uliloniambia ni jambo dogo sana kwake." Alisema bosi hiyo na kumshtua wenzake "Unasema kweli?" "Si hilo tu uliloniambia? Au kuna lingine? "Hilo tu mheshimiwa." "Basi ondoa shaka, Huyu kijana hata kama kuna lingine angetatua tu. Ameisaidia nchi kwa mambo mengi makubwa, sembuse hili tu la kijamii?" "Haya mheshimiwa namhitaji hata kesho aje ili nimpe mrejesho, faili na nimkabidhi wa wahusika ili aanze kazi."
"Okay, nikamwita asubuhi na kumwambia hilo." "Ahsante sana mheshimiwa." "Karibu Kamanda." Tayari alikuwa ameutua mzigo ambao ulikuwa unataka kumuelemea. Kelele za wananchi kuhusu kutekwa kwa mtoto kulimsumbua na alidhani kina Chacha alikuwa wamefika mbali, kumbe walikuwa wanapigwa chenga na watekaji. Alimuamini mwenzake Bosi wa Usalama kwani hajawahi kumuangusha hata mara moja.
Bosi wa Usalama naye baada ya kumsikiliza kwa makini alijua nani ya kumpa ili kuutatua mkasa huo tata.
Alitabasamu mwenyewe akimfikiria mtu ambaye atamkabidhi kazi hiyo, kwani hupenda mno kupeleleza, kusaka na kukamata wahalifu kwenye mazingira magumu kama hayo.
"Kama alifanya kazi ngumu za kuisaidia nchi, ndani na nje ya Tanzania, hii ni rahisi zaidi kwake. Nadhani haitochukua hata wiki mbili." Akajisemea mwenyewe.
Akainua mkono wake kutaka kumpigia simu, lakini kama kuna sauti ikamwambia asubiri mpaka kessho yake kwani muda ulikuwa umekwenda mno. Akaangalia saa yake ya mkononi. Ikamuonyesha ni saa 10:00 jioni, muda ambao hata yeye mwenyewe anatakiwa aondoke ofisini.
Itaendelea Jumapili
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED