USWAHILINI kuna mambo! Yoyote ambaye anaishi maeneo yenye mkusanyiko wa jamii atakubaliana na hili.
Ni kweli kuwa kuishi sehemu zenye hadhi au wenyewe wanaita 'Uzunguni', kuna raha yake, lakini pia kuna karaha yake pia. Na tunaoishi kwenye mkusanyiko wa jamii, wenyewe wanaita 'Uswahilini' kuna uzuri wake na ubaya wake pia.
Nikianza 'Uzunguni' ni sehemu za gharama, ambako huishi watu wenye nyadhifa, viongozi na matajiri na wengine wanaofanana na hao. Maeneo kama haya huwezi kukuta watu wanachanganyika kama vile kukutana sana kwenye shughuli za kijamii au kwenda kusalimiana na kujuliana hali mara kwa mara.
Huko kila mtu na lwake. Hii inasababisha kutofuatiliana, ambapo kila mtu anafanya lake ambalo mwingine wala hana mpango nalo. Hataki kujua wala kufuatilia. Maana yake hawafuatiliani. Huo ndiyo uzuri wake.
Ubaya wake sehemu kama hizo ni upweke. Mtu anaweza kupata tatizo kubwa linalohitaji ushauri, lakini akaukosa na kuamua kufanya kitu chochote kwa sababu ya upweke. Ni sehemu ambazo mtu anaweza kudhuru mtu au kujidhuru kutokana na msongo wa mawazo, au kupatwa na kitu kidogo tu ambacho huko uswahilini ni cha kawaida sana, lakini huyu wa uzunguni kwa sababu hajawahi kumuona yoyote kimemkuta, akaona ana mkosi kuliko watu wote duniani, akaamua kujidhuru. Kwa bahati mbaya sana hakuna watu wa kuja kumpa ushauri kutokana na mazingira ya eneo lenyewe.
Uswahilini sasa. Huko ni sehemu ambazo kama vile wanaishi pamoja. Nyumba zinabanana na watu wanaishi kijamaa.
Uzuri wa uswazi, ni kwamba watu wana ushirikiano ukitokea ugonjwa, msiba, au tatizo lolote lile. Wana tabia ya kusaidiana. Hata jirani anapopata tatizo la kisaikolojia, wapo wazee na wengine ambao wataifanya hiyo kazi kwa kumpa mifano hai ya watu wengi ambayo yamewapata na yamepita na maisha yanaendelea kama kawaida.
Uswahilini 'stresi' utake mwenyewe. Ni sehemu zilizochangamka kwa kila kitu. Kama nilivyosema mwanzo kila kitu kina faida na hasara. Uswahili tatizo lake ni watu kufuatiliana na baadhi yao kuwa na roho mbaya ya mafanikio ya wenzao. Unapoonekana maisha yako yameanza kunyoona tu tatizo. Kuna watu watakununia bila sababu yoyote.
Hujawahi kugombana nao, lakini wanaweza chuki ambayo huwezi hata kujua chanzo chake ni nini? Wao maisha ya watu na hasa mahusiano ya mapenzi wa wenzao yanawauma mno. Watachohitaji usiwe na maisha mazuri na wala mpenzi wa kudumu ili wapate cha kuongea. Ukiishi uswahilini jiandae au uwe na uwezo wa kukabiliana na fitina za chini chini na dha dhahiri kutoka kwa baadhi ya watu wanaokuzunguka, wengine ni marafiki zako kabisa.
Mwanamuziki Tshimanga Kalala Asossa, katikati ya miaka ya 1980, akiwa na bendi ya Orchestra Maquis Original, alitunga kibao kinachoshabihiana na tabia hizi za uswazi.
Maudhui ya wimbo huu unamuelezea kijana mmoja mpole, mcheshi, anayeongea na kila mtu, lakini kuna baadhi ya majirani wanampiga zengwe kwa madai kuwa anaringa sana. Mwenyewe anatambua hili na kuanza kuwalalamikia.
Wimbo huu unaimbwa hivi; "Usiku wa jana sikulala, nasikia moyo unauma, wasiwasi mwingi roho inauma.
Kumbe ilikuwa utabiri, njama njama za majirani ooh mama, wanasema naringa oooh sana, wao wanaona bora niage dunia kabisa oooh mama.
Kwa maneno ya chuki wamenizungaka oooh, bure ooh, bure oooh, bure ooh, wamepigana nami bure, wamenitukuza mabaya badala ya mema bure oooh, bure oooh, bure.
Na chuki badala ya upendo wangu, nilikuwa na utu kwao mama, wanionapo hutikisa vichwa vyao,Walijivika laana kama kanzu, ikawaingia mioyoni mwao."
Haya ni malalamiko ya kijana ambaye aliwaona baadhi ya majirani zake watu wazuri, kumbe walikuwa nyoka kwake.
"Bahati yangu yangu kweli oooh, iyolele, na matatizo yote Mungu anajua, ubaya na wema wangu wote iyolele, Ndio umeniponza. Machozi yanidondoka iyolele, nakosa hata la kufanya. Kusemasema sikuzoea iyo mama,yote kwa Mungu baba eeeh."
Kwa yote ambayo anafanyika anamuachua Mwenyezi Mungu, yeye ndiye hakimu wa haki. Huko ndiko kunaitwa 'Uswahilini.' Kuishi ni kama uko vitani.
Tuma meseji 0716350534
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED