Yanga Princess, Simba Queens, kazini leo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:25 AM Feb 04 2025
Kikosi cha Simba Queens
Picha: Mtandao
Kikosi cha Simba Queens

TIMU za soka za Wanawake, Yanga Princess na Simba Queens, leo zitashuka kwenye viwanja tofauti Dar es Salaam, kusaka pointi tatu ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya mbio za umalkia wa mchezo huo nchini.

Mabingwa Watetezi wa ligi hiyo, Simba Queens, watashuka Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, maeneo ya Mwenge, kucheza dhidi ya Ceasiaa Queens, katika mchezo wa raundi ya 12 ya ligi hiyo.

Katika mchezo huo, Simba Queens itahitaji pointi tatu ili kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, wakiwa na lengo lao la kutaka kulitetea tena taji hilo.

Timu hiyo iko kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 31, ambapo kama ikishinda itafikisha pointi 33, ikibakisha michezo sita tu ili kujua hatima yao.

Yanga Princess
Inacheza na Ceasiaa Queens, ambayo ipo nafasi ya saba kwenye msimamo ikiwa na pointi 10.

Kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, kutakuwa na mchezo mwingine wa ligi hiyo ya wanawake ambapo Yanga Princess, itakuwa mgeni wa Mashujaa Queens.

Mechi hiyo inatabiriwa kuwa ngumu zaidi kutokana na timu zote kuwa na pointi 18, hivyo yoyote itakayoshinda itakaa juu ya mwenzake.

Yanga Princess, inashika nafasi ya tatu, huku Mashujaa Queens ikiwa ya nne, zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Mbali na mechi hizo, JKT Queens inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo, itashuka Uwanja wa Kituo cha TFF Kigamboni, kucheza dhidi ya Mlandizi Queens, huku Bunda Queens ikiwa nyumbani Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara, kucheza dhidi ya Gets Program, na wakati huo huo katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, Alliance Girls itakuwa na shughuli pevu dhidi ya Fountain Princess.