Yanga kuivaa Tabora United robo fainali FA

By Saada Akida , Nipashe
Published at 06:22 AM Apr 18 2024
Wachezaji wa Yanga wakishangilia moja ya gilo katika mchezo wao Ligi Kuu Tanzania Bara.
Picha: Maktaba
Wachezaji wa Yanga wakishangilia moja ya gilo katika mchezo wao Ligi Kuu Tanzania Bara.

DROO ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Benki ya CRBD (CRDB Federation Cup), imefanyika jana ambapo bingwa mtetezi wa michuano hiyo Yanga, atamkaribisha Tabora United katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi Dar-es-Salaam.

Michezo mingine ni Azam FC wakiwa nyumbani wataikaribisha Namungo FC katika dimba hilo la Azam, Coastal Union dhidi ya Geita Gold FC Uwanja wa Mkwakwani jiji Tanga na Ihefu FC watakuwa nyumbani dhidi ya Mashujaa FC, Uwanja wa Liti mkoani Singida.

Michezo hiyo ya robo fainali  inatarajiwa kuchezwa kati Mei 2 hadi 4, huku nusu fainali ikitarajiwa kuchezwa Mei 18 hadi 19 na fainali itapigwa Juni 2, mwaka huu.

Nusu fainali ya kwanza itachezwa kati ya mshindi wa mchezo kati ya Azam FC dhidi ya Namungo FC atacheza na mshindi kati ya Coastal Union dhidi ya Geita Gold FC. 

Kwa upande wa nusu fainali ya pili itakuwa kati ya mshindi wa Ihefu FC dhidi ya Mashujaa FC  kati ya mshindi wa mechi ya  Yanga na Tabora United.

Kwa mujibu wa Meneja wa Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Baraka Kizunguto, nusu fainali ya kwanza ya itachezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza huku wakisubiri taratibu zingine juu ya uwanja utakaochezwa nusu fainali ya pili 

“Fainali itachezwa Manyara katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, timu zote zinazocheza robo fainali zinatakiwa kujiandaa,” alisema Kizunguto.