Ruto aliagiza Jeshi kuokoa waathirika wa mafuriko

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:48 AM May 01 2024
Mafuriko nchini Kenya.
PICHA: MAKTABA
Mafuriko nchini Kenya.

RAIS wa Kenya, William Ruto ameliagiza jeshi la nchi hiyo kuwahamisha wananchi ambao wamekumbwa na mafuriko yaliyoua watu 171 kufuatia mvua kubwa zaidi kulikumba taifa hilo la Afrika mashariki tangu mwezi Machi.

Rais Ruto, ambaye amewatembelea waathirika wa mkasa huo baada ya kuongoza kikao cha Baraza la Mawaziri mjini Nairobi, ambapo amesema serikali imechora ramani ya vijiji ambavyo vipo hatarini kukumbwa na mafuriko, wakati tahadhari ya mvua ikiendelea kutolewa.

Waokoaji wanaendelea kuitafuta miili ya waathirika baada ya mvua kusababisha mafuriko na maporomoko makubwa ya ardhi kuwahi kushuhudiwa kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki katika miaka ya karibuni.

Taarifa zinasema kuwa idadi ya watu ambao hawajulikani walipo ilikuwa ikiendelea kuongezeka.

Inasemekana zaidi ya watu 190,000 wameyakimbia makazi yao wakiwemo 147,000 katika mji Mkuu wa Nairobi, huku Idara ya Hali ya Hewa nchini himo ikisema bado maeneo kadhaa yalikuwa yakitarajiwa kupata mvua kubwa katika siku zijazo.