Yanga hasira zote Ligi Kuu Bara, FA

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:11 AM Jan 23 2025
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe
Picha: Mtandao
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe

BAADA ya kuondolewa katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kikosi cha Yanga kimeingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya mashindano ya Kombe la FA dhidi ya Copco FC utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Yanga iliiaga michuano ya kimataifa baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Kundi A nyuma ya vinara Al Hilal ya Sudan, MC Alger ya Algeria huku TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo), ikiburuza mkia.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara walihitaji ushindi wa aina yoyote katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi, lakini matokeo ya sare ya bila kufungana yaliwafaidisha MC Alger ambayo ilifikisha pointi tisa na Yanga kufikisha pointi nane, Al Hilal alimaliza kileleni akiwa na pointi 10.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema baada ya kukosa bahati ya kutinga hatua ya robo fainali, akili na nguvu zao sasa wamezielekeza kwenye mchezo wa Kombe la FA pamoja na mechi ya kiporo ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa Februari Mosi, mwaka huu.

"Timu kwa sasa imerejea kambini baada ya mapumziko ya muda mfupi, tuna mechi ya Kombe la FA dhidi ya Copco, ni mechi muhimu kwa ajili ya kurejesha nyuso za furaha kwa mashabiki wetu, tunawaahidi  tutarudi kwa nguvu kubwa.

Tutahakikisha tunarudi kutetea makombe yetu yote, kuanzia hili la FA, hadi Ligi Kuu, hatuwezi kushindwa kutinga robo fainali ya Afrika, halafu pia tukapoteza makombe yetu, haya ndiyo yatatupoza machungu, na wataturudisha katika michuano kama hiyo msimu ujao," alisema Kamwe.

Wakati huo huo, Yanga imesema kauli iliyotolewa na Kocha Mkuu wa timu yao, Sead Ramovic, kuhusu ubora wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kutupwa nje katika michuano ya CAF, haikueleweka vyema kwa wadau.

Kamwe alisema kumekuwa na mijadala mingi katika mitandao ya kijamii, televisheni na vipindi vya michezo, ikiwamo matamko ya baadhi ya watu wa mpira kujibu alichosema, lakini wengi wamekuwa wakijibu kitu ambacho walikuwa hawajaelewa alichokimaanisha kocha huyo.

Alifafanua Ramovis hakusema Ligi ya Tanzania ni dhaifu, kama wengi walivyoelewa na 'kukazia hapo', badala yake alimaanisha uharaka wa matukio uwanjani katika mechi za ligi hiyo.

"Nadhani neno, 'intensity', ndiyo limewachanganya watu, ukilitafsiri huwezi kupata neno udhaifu, badala yake ni ukali, kasi na uharaka na matukio na ndicho alichomaanisha. Mpira una matukio mawili, timu inapokuwa na mpira na inapokuwa haina, sasa ni vipi timu inajibu kwa vitendo inapokuwa naona mpira na ambapo haina mpira kwa uharaka.

Hiki ndicho alichosema kocha wetu na hata kwenye ligi mbalimbali Ulaya, Ligi ya England ina uharaka wa matukio uwanjani na kasi, kuliko ya Ufaransa, lakini huwezi kusema ni dhaifu," alisema Kamwe.

Aliongeza ubora wa ligi na uharaka wa matukio katika ligi husika ni vitu viwili tofauti, hivyo baadhi ya wadau wakiwamo wachambuzi waache kumshutumu kocha wao kwa sababu alichokisema ni sahihi na wao ndiyo wanaopotosha.

"Tunapaswa kuwa wakweli kuhusu Ligi ya  hapa Tanzania, ugumu unaokutana nao unapocheza dhidi ya timu nyingine za Tanzania sio wa kiwango kikubwa sana. Ukiona Ligi za Algeria, Afrika Kusini, Morocco, Tunisia, tunahitaji nguvu na kasi hiyo ya juu ili kushindana na tuzoee hali hiyo.

Ukali na kasi ya ligi ya Tanzania, ni mdogo sana ukilinganisha na nchi hizo, wao ligi yao ni ngumu na kila timu kali sana, tunahitaji ugumu kama wa ligi hizo ili tushindane," aliongeza.

Alisema pia siku hazifanani na viwango vya wachezaji hubadilika.

"Niwaambie tu Wanayanga wote watulie, tulikuwa na siku mbaya kazini, hatukucheza kwa kiwango chetu kwa asilimia 100, nilizungumza na wachezaji wote baada ya ile mechi na niliwaambia laiti tungerudia kucheza asilimia 60 tu ya kiwango tulichoonyesha dhidi ya Al Hilal Omdurman kule Mauritania, MC Alger ilikuwa inakufa kwa Mkapa, lakini ndiyo mpira, watu wanaweza kuamka vizuri leo, kesho wakaamka vibaya," aliongeza.